KORTI YAAMURU WATUHUMIWA KESI NYARA ZA SERIKALI WAKAMATWE

na Mwandishi wetu, Rufiji. MAHAKAMA ya Kibiti iliyopo wilayani Rufiji, mkoani Pwani imetoa hati ya kukamatwa washitakiwa watatu katika kesi ... thumbnail 1 summary
na Mwandishi wetu, Rufiji.
MAHAKAMA ya Kibiti iliyopo wilayani Rufiji, mkoani Pwani imetoa hati ya kukamatwa washitakiwa watatu katika kesi ya kukutwa na nyara za serikali kwa kushindwa kufika mahakamani bila sababu za msingi.

Walioamriwa kukamatwa, ni Shilu Mtimbula, Joseph Chilumba na William Mgaya.
Akitoa amri hiyo mwishoni mwa wiki, Hakimu wa Wilaya, Muhidin Matitu, alisema mahakakama haina taarifa ya sababu za kushindwa kwao kufika mahakamani, hivyo akawaagiza maofisa watendaji wa vijiji wahakikishe wanawakamata na kuwafikisha mahakamani.
Akiahirisha kesi hiyo, Hakimu Matitu alisema itatajwa Septemba 26, mwaka huu.
Awali, Mwendesha Mashitaka, Gabikwa Ushomile, alidai washitakiwa walikamatwa na nyara hizo muda na maeneo tofauti ndani ya wilaya hiyo.
Mbali ya hao, wengine waliofikishwa mahakamani hapo kwa kosa hilo, ni Jumanne Ligenge, Scolastica Ernest, Hamis Seleman, Hassan Jumanne na Juma Lubanga.
Kwa mujibu wa Ushomile, kesi hiyo imeshindwa kuanza kusikilizwa kwa sababu jalada la upelelezi bado lipo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa kwa uchunguzi zaidi.
Wakati huo huo, baadhi ya wakazi wa Rufiji wameiomba serikali kuharakisha kusikiliza na kuamua kesi zinazohusu watu waliokamatwa na nyara za serikali au ujangili.
Akizungumza mjini Dodoma hivi karibuni, Mbunge wa Rufiji, Seif Sulemain Rashid, alishauri Idara ya Mahakama kuharakisha usikilizaji na uamuzi wa kesi zinazohusu nyara za serikali.
Aidha, alipendekeza kuanzishwa kwa mahakama maalumu itakayokuwa ikishughulikia watu wanaopatikana na nyara za serikali.
Chanzo: Tanzania Daima