Vita
ya ujangili na uhifadhi wa wanyama kwa kiasi kikubwa inafanywa na watu wa ngazi
za chini yaani walioko kwenye maeneo husika, achana na hawa viongozi wetu
wanaokaa maofisini na kuagiza hili mara lile, nzungumzia wale askari
wanyamapori walioko kwenye hifadhi wanaopurukushana na majangili usiku na
mchana.
Hata
hivyo idadi ya askari wanyamapori na uwezo wao kimafunzo si yakuridhisha sana
katika hifadhi zetu nchini jambo lililofanya kuwepo jitihada za maksudi
kuongeza idadi ya askari hao ambapo jumla ya Askari 100 waliofuzu usaili wa
awali wa ajira ya uaskari wanatarajiwa kuanza rasmi mafunzo maalum ya mbinu za
medani katika hifadhi ya Taifa ya Katavi ili kuongeza nguvu katika idara ya
Wanyamapori kukabiliana na vitendo vya ujangiri nchini.
Afisa
habari wa Shirika la hifadhi za Taifa TANAPA Paschal Shelutete aanasema kuwa
mafunzo hayo maalum ya miezi mitatu kwa askari wake ni utaratibu mpya ulioanzishwa
na TANAPA katika kuajiri Askari wakakamavu na wenye mbinu za kuzibiti vitendo
vya ujangiri vinavyoendelea hivi sasa.
TANAPA
imeandaa mafunzo hayo ili kukabiliana na upungufu wa askari hao lakini pia
kuongeza nguvu katika kukabiliana na majangili katika hifadhi za Taifa, mafunzo
ambayo yanawalenga askari waliopitia mafunzo ya uaskari katika jeshi la kujenga
taifa na chuo cha wanyamapori kilichopo Pasiansi mkoani Mwanza.
Mbali
na kuwaimarisha askari wake Shelutete amesema TANAPA kwa kushirikiana na Vyombo
vya Dola wameelekeza nguvu katika kuwachunguza na kuwachukulia hatua za
kinidhamu na kisheria Wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa wanaobainika
kujihusisha na vitendo vya ujangiri.