Fastjet yatakiwa kutazama upya gharama za mizigo

Katikati ni Meneja wa Uwanja wa Ndege mkoa wa Mwanza Bi. Esta Madale akiwa na wafanyakazi wa kampuni ya Fastjet. Serikali imeitaka ... thumbnail 1 summary
Katikati ni meneja  wa  uwanja wa ndenge mkoa wa  mwanza,Bi, Esta Madale akiwa  na wafanyakazi wa kampuni  ya Fastjet.
Katikati ni Meneja wa Uwanja wa Ndege mkoa wa Mwanza Bi. Esta Madale akiwa na wafanyakazi wa kampuni ya Fastjet.

Serikali imeitaka kampuni ya ndege ya Fastjet inayofanya biashara zake nchini na nje ya nchi kutazama upya gharama za utozaji wa mizigo ya abiria ili iweze kuendelea kuwasaidia wananchi wenye uwezo wa chini kumudu kutumia usafiri wa anga hapa nchini na kuachana na msongamano wa matumizi ya barabara.  

James Chuwa ambaye ni Katibu Tarafa ya Ilemela aliyasema hayo kwenye hotuba, kwa niaba ya Mkuu Mkoa wa Mwanza kwenye ufunguzi wa ofisi mpya ya kampuni hiyo iliyofunguliwa leo katika uwanja wa Ndege wa Jiji la Mwanza .

Bwana Chuwa alisema kuwa kampuni hiyo imekuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wenye kipato cha chini katika kutumia usafiri huo, lakini changamoto kubwa imekuwa ni ongezeko la nauli kwa kusafirisha mizigo hali inayolalamikiwa na baadhi ya wasafiri na kutaka kuacha kutumia usafiri huo wa anga kwa kukimbia gharama za mizigo.

“Nafikiri kuna haja sasa kwa menejimenti ya fastjet kulitazama suala hili na kulitafutia ufumbuzi ili watanzania wengi waendelee kuwa waumini wa kampuni hiyo na kunufaika kwa kutumia usafiri wa anga kama wengine wanavyonufaika sanjari na kurahisisha shughuli zao za kimaendeleo za kufikia maeneno mbalimbali yenye fursa za kimaendeleo.” alisema Bwana Chuwa.

Naye mtumiaji wa kampuni hiyo ya usafirishaji bwana Daudi John alisema kuwa, tangia fastjet iingie Tanzania imekuwa kimbilio kubwa la wananchi wenye kipato kidogo tofauti na ilivyokuwa hapo awali, hali inayoongeza ushindani pamoja na ufanisi katika sekta ya usafiri wa anga.

Meneja wa uwanja wa ndege wa Mwanza Bibi Ester Madale alisema kuwa anajisikia fahari kwa uwanja huo kuwa na wasafiri wengi kwa sasa, hiyo yote imetokana na ujio wa fastjet iliyoweza kuhamisha wasafiri wengi toka kwenye usafiri wa mabasi na sasa kuhamia kwenye usafiri wa anga, hali inayowapa changamoto mamlaka ya uwanja huo kuboresha huduma zao.

Meneja wa fasj jet Mkoa wa Mwanza Bwana Vishal Dass Choudhry alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kukubali kuipokea vyema fastjet na kuendelea kutoa ushirikiano wa mambo mbalimbali ikiwemo kutoa eneo la ujenzi wa ofisi mpya ya fastjet katika eneo la uwanja wa Ndege wa Mwanza hali itakayosogeza huduma kwa jamii kwa ukaribu zaidi tofauti na hapoawali, ambapo wasafiri walilazimika kwenda mjini kupata huduma za kampuni hiyo.

Naye Meneja wa Biashara wa Kampuni hiyo Bi. Jean Uku alieleza kuwa, fastjet itaendelea kuwajali watanzania kwa kuboresha huduma zao sambamba na kupunguza bei za usafiri ili watanzania wengi waweze kusafiri na usafiri wa ndege kwa lengo la kurahisisha shugulizao na kufikia sehemu zenye fursa kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa opereshieni wa fastjet Bwana Sagar Charda alisema kuwa ili kuboresha maisha ya watanzania, kampuni hiyo ina mpango wa kuleta ndege kubwa zaidi aina ya Air Bus ili kufanya safari katika Nchi mbalimbali za Afrika na kuwaunganisha watanzania na miji ya kibiashara barani afrika.

Fastjet ilitangaza ofa maalumu kwa wasafiri watakaokata tiketi zao katika ofisi hiyo mpya pekee na kupata punguzo la nauli pamoja na kusafirisha begi pamoja na ndoo ya samaki bure kuelekea jijini Dar es Salaamu, hivi sasa kampuni hiyo itaanza safari zake katika miji ya Arusha, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.