Kumbukumbu ya miaka 18 toka kuzama kwa MV Bukoba

Meli ikiwa inazama na ikiwa imezungukwa na mitumbwi pamoja na boti ambazo zilisaidia kwenye uokoaji RIPOTI ya Tume ya Jaji Robert Ki... thumbnail 1 summary
Meli ikiwa inazama na ikiwa imezungukwa na mitumbwi pamoja na boti ambazo zilisaidia kwenye uokoaji

RIPOTI ya Tume ya Jaji Robert Kisanga, iliyochunguza chanzo cha ajali ya mv Bukoba, inasema usiku wa kuamkia siku ya ajali, meli hiyo ilipakia abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37.

Kati ya hao, 114 waliokolewa wakiwa hai; wakati 391 waliopolewa wakiwa wamefariki na kuzikwa katika makaburi ya Igoma, nje kidogo ya Jiji la Mwanza. Miili mingine ilichukuliwa na jamaa kuzikwa kwao. Jumla ya miili 332 haikupatikana.

Kila mwaka, ifikapo Mei 21, serikali inayosema haina dini, huongozana na viongozi wa madhehebu ya dini na waganga, kwenda eneo la ajali kufanya kumbukumbu.

Serikali ilishitaki aliyekuwa nahodha wa mv Bukoba, Jumanne Rume-Mwiru, (sasa marehemu), Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari Gilbert Mokiwa; aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo, na aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.

Meli ya Mv Bukoba ikiwa inazama.

Kesi hiyo Na. 22 ya mwaka 1998, ilianza kusikilizwa Mei 14 mwaka 2001. Miongoni mwa waendesha mashitaka katika kesi hiyo ni Eliezer Feleshi.Hukumu ya kesi ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Juxton Mlay (sasa mstaafu), Ijumaa, 29 Novemba 2002, majira ya saa sita mchana.

Washitakiwa wote walishinda kesi, kufuatia hukumu ya kurasa 118 iliyosomwa kwa dakika 160 na Jaji Mlay kusema, mv Bukoba ilizama kwa sababu haikuwa na uwiano wa majini na siyo uzembe wa washitakiwa.

Serikali iliahidi kukata rufaa; lakini hadi leo majaliwa ya rufaa hiyo hayajulikani; na baadhi ya washitakiwa wamefariki dunia bila kujua hatma ya kesi hiyo wala stahili zao.

Kwa kipindi kirefu, mv Bukoba ilikuwa ‘kaburi’ lenye kuelea katika Ziwa Victoria. Ilikwishapigwa marufuku kufanya safari kwa kuwa haikuwa na viwango vya ubora wa kuwa majini.

Makaburi ya Igoma ambako wahanga wa Mv Bukoba walikozikwa

Meli hii ilijengwa na kampuni ya Kibelgiji; ikazinduliwa 27 Julai 1979. Siku ya uzinduzi, ilibainika haikuwa thabiti na ilikosa uwiano.


Chanzo: JF