MMOJA WA WASHIRIKI WA MAISHA PLUS/MAMA SHUJAA WA CHAKULA APOTEA, SEMINA ZAENDELEA.

Kama kawaida wanakijiji walianza siku kwa kufanya mazoezi ya viungo ili kuweka miili yao sawa tayari ku... thumbnail 1 summaryKama kawaida wanakijiji walianza siku kwa kufanya mazoezi ya viungo ili kuweka miili yao sawa tayari kukabiliana na shughuli za siku hiyo. Baada ya mazoezi kumalizika wanakajiji  walibaini mmoja wao ametoweka katika mazingira ya kutatanisha bila kujua ameelekea wapi. Hofu ilitanda katika kijiji cha Maisha Plus huku wanakijiji wakijiuliza kimetokea nini kwa mwenzao Anna Mwanilyela Chrisant kutoka Katavi kwani wengine walidhani amekufa, wengine walidhani ametoroka, wengine walidhani ni mchezo umefanyika na baadaye anaweza akarudi  na wengine walidhani amechukuliwa na Epheta Msiga ambaye huonekana kwa nadra sana hapo kijijini. Kuonekana kwake ni ishara ya mwanakijiji mmoja kuaga mashindano hayo. Kwa kweli wanakijiji wote hawakuwa na jibu kamili ya wapi mwanakijiji huyo ameelekea. Hofu ilitanda zaidi pale askari polisi wapofika katika kijiji cha Maisha Plus baada kupewa taarifa ya kupotea kwa mwanakijiji huyo na kufanya mahojiano na uongozi wa kijiji ili kupata taarifa zitakazosaidia kumtafuta mwanakijiji aliyepotea.
Mahojiano yalifanyika na mwanakijiji anayedhaniwa kapotea katika mazingira ya kutatanisha na kumkuta katika hali ya usalama na alikuwa na haya kusema ‘washiriki wasiwe na hofu kwani kilinifanya leo niage mashindani ni kutokana na afya yangu kuendelea kuwa mbaya. Nilitegemea nitapata nafuu nilivyoingia humu nikajua nitapona taratibu laikini siku zilivyokuwa zinazidi kwenda najiona hali yangu inakuwa si nzuri kwani nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya mgongo na kiuno hasa nyakati za usiku nikaona vema niage mashindano nikapate mtibabu zaidi ingawa nilitamani niwepo mpaka mwisho. Washiriki waliobaki kwa kweli nawaomba wamtangulize Mungu kwani hakuna jambo lisilowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu na wadumishe amani, upendo kati yao na wapeane mambo mazuri ya kielimu ili iwasaidie wao na jamii kwa ujumla’. Anna aliweza kujifunza mambo mbalimbali kutokana na ushirki wake kwa wiki moja ikiwemo masuala ya kijinsia, sheria na haki za wanawake hasa umiliki wa ardhi ambao bado ni changamoto kwa wanawake wengi. Vile vile jamii inayomzunguka itafaidika na stadi alizopata za kutengeneza sabuni, mafuta ya mgando, bustani ndogo ndogo nyumbani na utunzaji wa mazingira.
Mgongano kijijini  
Tofauti ilitokea baina ya wanakijiji ambapo mama shujaa mmoja alidai kuwa baadhi ya wanakijiji wenzake wanamsema vibaya hivyo kuripoti katika uongozi wa kijiji. Viongozi hao walichukua jukumu la kuwaita wale wote waliohusika na kuomba msamaha kwa mama huyo kwa kile walichokifanya. Zoezi hili liliambatana na mama shujaa aliyesemwa vibaya na wenzake kukabidhiwa mfano wa mtoto mdogo kama ishara ya kumaliza tofauti zao ili waweze kuendelea na maisha kama kawaida. Hivi ndivyo wanakijiji wa Maisha Plus wanavyoishi kwa amani, upndo na bila kuwekeana kinyongo kuendeleza ugomvi ndani ya kijiji.   
Mabadiliko ya Tabia nchi
Mabadiliko ya tabia nchi ni moja ya mada zilizotolewa kwa washiriki wa muhula wa nne wa Maisha Plus. Mada hii ilitolewa na wawakilishi kutoka Ekama Development akiwemo Roselyn Kaihula na Hilda Mashauri. Ekana Development ni shirika lisilo la kiserikali lililojikita katika kuwajengea uwezo wanajamii kupitia utafiti hususan katika masuala ya haki za wanawake na watoto chini ya umri wa miaka 18.
Mwakilishi kutoka Ekama Development Hilda Mashauri alitoa maelezo na kusema Ekama Development hushirikiana na Oxfam katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, usawa wa kijinsia na kilimo rafiki kinachozingatia hali ya eneo husika ili kuleta tija kwa mkulima. Alisema wamejiandaa vema kuendesha mashindano kwa kuwauliza maswali washiriki wa Maisha Plus na Mama Shujaa ambapo tayari timu mbili zimeshaundwa kwa mashindano hayo yatakayofanyika siku ya Jumanne wiki ijayo. Timu hizo ni Mandela na Mwalimu Nyerere. Zawadi zitatolewa kwa mshindi wa shindano hilo ingawa aina ya zawaida haukutajwa na kubaki kuwa siri mpaka siku hiyo ya makabidhiano kama ilivyopangwa na waandaaji wa shindano hilo. Pia alisifu kinamama Shujaa kwa umahiri wao kueleza kilimo rafiki na namna gani wanavyotumia kilimo hicho katika maeneo yao.
Msemaji wa timu ya Mandela Ally Thabit alisema tumejitayarisha kuwa washindi kwani tumeshajipanga vema na kuteua viongozi ambao watakao tuongoza na kuhakikisha tunaibuka na ushindi siku ya Jumanne. Vile vile wakina mama Shujaa nao hawapo nyuma wanatushirikisha na kutupa uzoefu waliokuwa nao katika masuala ya kilimo kwenye maeneo yao ili kujidhatiti vizuri zaidi katika kuyajibu maswali tutakayoulizwa siku hiyo ya mashindano.
Naye msemaji wa timu ya Mwalimu Nyerere Bakari Khalid alisema hakuna sababu ya kushindwa kuwa mshindi siku ya Jumanne kwa kuwa maswali yanayoulizwa yanatokana na kile tulichojifunza na pia tumepewa kitini kinachozungumzia zaidi masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na kilimo rafiki. Pia naamini kupitia kipindi hiki jamii ya kitanzania itakuwa imejifunza mabadiliko ya tabia nchi ni nini na namna kilimo rafiki kinavyoweza kumnufaisha mkulima na jamii kwa ujumla wakati huo huo unalinda mazingira.