Kulikuwa na
mdahalo kijijini ulioendeshwa na wataalamu wa kilimo kutoka ANSAF (Agricultural
No State Actors Forum) ambalo limejikita katika kushawishi serikali na wadau wa
kilimo, kusaidia wakulima wadogo wadogo, kuimarisha fursa zilizopo na kuongeza
myororo wa thamani katika kilimo. Mdahalo huu uliongozwa na Mkurugenzi wa ANSAF
Audax Rukonge na wanajopo wengine Elias Rwekeza Mkurugenzi Mtendaji wa
OppAccess Co. Ltd iliyopo Morogoro, Mwenyekiti mwanzilishi wa Tanzania Graduate
Farmers Association Stephano P. Kigazi, Ernest Likokoo kutoka TGFA, Brendalinny
John na Epiphania Mngazija kutoka ANSAF. Katika mdahalo huu upatikanaji wa
taarifa sahihi katika kilimo umetiliwa mkazo ili kumuweka mkulima katika hali
ya kuweza kufanya maamuzi sahihi yanayohusu kilimo na kuweza kumpatia tija
zaidi.
Vile vile wanakijiji cha
Maisha Plus walipata fursa ya kuweza kupata maelezo ya hatua zinazotakiwa kufuatwa
katika ujenzi wa jiko la gesi kuanzia ujenzi wenyewe, mitambo na matumizi yake,
gesi yenyewe inavyozalishwa na hatimaye tope chujio. Tope chujio ni hatua ya
mwisho ya uzalishaji gesi ambayo ni mbolea nzuri na yenye ubora kwa mimea
tunayozalisha. Darasa hili lilitolewa na Richard Daniel ambaye alikuwa bega kwa
bega na wanakijiji cha Maisha Plus katika hatua zote za ujenzi akisaidiana na
mwanadada Theopista Mapunda katika hatua ya awali.
Jiko hili tayari
lilizinduliwa rasmi na mama Tunu Pinda na kuanza kutumika na wanakijiji. Kila kaya
ya kijiji cha Maisha Plus hupata fursa ya kupika katika jiko hilo la gesi na
kupunguza adha ya kutafuta kuni wakati huo huo kutunza mazingira kwa kuepuka
kukata miti ovyo.
Ile azma ya kundi
lililoshinda kutumikiwa na makundi yaliyoshindwa imetimia baada ya kundi hilo
kuibuka kidedea katika kutambua vitu mbalimbali huku wakiwa wamefunikwa macho
kwa kitambaa cheusi.
Kila mwanakikundi alipewa mjakazi wa kumtumikia na kufanya
yale yote aliyoagizwa na mfalme au malkia kwa kuwa kundi hilo walipewa cheo cha
malkia kwa wanawake na mfalme kwa wanaume. Wafalme wengine waliamuru wajakazi
wao wawabebe mahali popote waendapo hapo kijijini kama ilivyokuwa kwa mfalme Said
Rashid kutoka Uganda alimtaka Asumta Mwingira wa Tanzania atembee naye popote
pale aendapo. Kwa malkia Flora John wa Tanzania alimtaka Caron Abisai kutoka
Kenya amwimbie na kumpigia gitaa ili apate kuburudika. Wanakijiji walikuwa na
pilika pilika za hapa na pale kuwatumikia wafalme na malkia kijijini hapo.