Katibu Mkuu Kiongozi Balozi, Ombeni Sefue, amewataka Watumishi wa Umma
kuwa wabunifu katika kutoa huduma kwa wananchi ili kuleta ufanisi uwazi
na uadilifu.
Aliyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki
ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja
jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwa wiki moja yakiwa
na Kauli Mbiu isemayo ’’ Mkataba wa Msingi wa Kanuni za Utumishi wa
Umma Barani Afrika ni Chachu ya Kuimarisha Utawala Bora na Uendeshaji wa
Shughuli za Serikali kwa Uwazi’’yamewapa fursa Watumishi wa Umma
kubadilishana uzoefu na wananchi wapatao laki tano.
Aidha,
Maadhimisho hayo yaliyoambatana na utoaji tuzo kwa washiriki waliofanya
vizuri katika vipengele mbalimbali, Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) wamekuwa kumi bora kati ya taasisi 88 zilizoshiki
kwenye maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma katika kipengele cha
ubunifu.
Wakala wa huduma wa Misitu Tanzania ( TFS) imetajwa
kufanya vizuri katika kipengele cha ubunifu wa kuzuia moto kwa
kutumia njia ya kisasa inayowezesha kugundua moto mara tu unapoanza
kuwaka mahali popote nchini.
Hivyo ubunifu wa teknolojia hiyo ya
kuzuia moto itasaidia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupunguza
tatizo la moto ambalo limekuwa likiteketeza misitu mingi nchini.
‘’Wananchi wana matumaini makubwa sana na ninyi watumishi wa Umma hivyo
wahudumieni vizuri hii itasaidia kupunguza malalamiko katika ofisi za
umma’’ Balozi Sefue, alisisitiza.
Alisema kila Mtumishi wa Umma
lazima ahakikishe anakuwa mbunifu ili kuweza kutimiza malengo yake
aliyakusudia na aliwakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi
ya watumishi kila mwaka.
Katibu Mkuu Kiongozi aliwaasa Watumishi
Umma kuwa waaminifu na wachapa kazi kwani Maadhimisho ya Wki ya
Utumishi wa Umma yamemsaidia kila Mtumishi Umma kuijtazama na
kujitathmini katika utendaji wake wa kazi wa kila siku.
Aidha Wizara
ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake zilizoshiriki kwenye Wiki ya
Utumishi Umma ikiwemo Bodi ya Utalii Tanzania, Chuo Cha Taifa cha
Utalii, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania zimepata fursa ya kuwashirikisha wananchi kwa kutoa maoni yao
jinsi ya kuboresha huduma wanazozitoa kwa lengo la kuhakikisha Maliasili
zilizopo nchini zinalindwa na kuhifadhiwa kwa gharama yoyote kwa
kuwashirikisha wananchi kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.