Ofisa
mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) amefariki dunia
na mwingine amesagika mguu baada ya mawe kuporomoka wakati wakipanda
Mlima Kilimanjaro katika mazoezi. Wanajeshi hao ni miongoni mwa maofisa
263 wa JWTZ waliopanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika kwa
makundi kuanzia Julai 12, mwaka huu kupitia njia ya Rongai iliyopo
wilayani Hai.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilieleza kuwa tukio hilo
lilitokea jana saa 10:00 alfajiri katika urefu wa mita 5,000 kutoka
usawa wa bahari wakati maofisa hao wakitoka eneo la Hans Meyer
wakikaribia kilele cha Gilmans.Mkuu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro
(Kinapa), Erastus Lufungulo alithibitisha jana kutokea kwa maafa hayo
na kueleza kuwa mawe hayo yaliporomoka kutoka juu ya Hans Meyer na
kushuka hadi eneo la Jamaica.
Aliyefariki dunia katika ajali hiyo wametajwa kuwa ni Cadet MT 104948
Malata Thomas Kitene (26) baada ya kupata majeraha ya kichwa na Cadet MT
105896 Gabriel Makenge (32) ambaye amevunjika na kusagika mguu wa
kushoto.
“Baada ya kupata taarifa za tukio hilo, kikosi chetu cha uokoaji
kilikwenda eneo la tukio na kushiriki kazi ya uokoaji, lakini taarifa
zaidi kuhusu ziara ya maofisa hao mnaweza kupata kwa wasemaji wa JWTZ,” alisema.
Hata hivyo, msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo.
Majeruhi pamoja na maiti ya ofisa hao waliteremshwa kutoka kileleni jana
saa 4:00 asubuhi na kupelekwa moja kwa moja Hospitali ya Rufaa ya KCMC
iliyopo mjini Moshi.
Taarifa zaidi zilisema maofisa hao walipanda mlima huo ikiwa ni utaratibu wa kila mwaka kwa ajili ya mazoezi ya ukakamavu.