Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ametangaza kufuta vitalu vyote vilivyokuwa chini ya Kampuni ya Green Miles Safaris Ltd kutokana na kukiuka sheria za uwindaji nchini, huku akiifuta Idara ya Wanyamapori.
Uamuzi huo wa Serikali, umekuja siku chache baada
ya Mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa kuonyesha video
inayoihusisha kampuni hiyo na ukiukaji wa sheria na taratibu za
uwindaji.
Awali, Msigwa ambaye pia ni Waziri Kivuli wa
Maliasili na Utalii alitoa madai hayo Mei 14, mwaka huu wakati wa
uwasilishwaji wa bajeti ya wizara hiyo mjini Dodoma.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam, Waziri Nyalandu pia alitangaza kuifuta Idara ya Wanyamapori
na kuunda Mamlaka ya Wanyamapori ili kuimarisha ufanisi katika sekta
hiyo.
“Kufuatia tuhuma zilizowasilishwa bungeni kwa njia
ya ushahidi wa DVD na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Peter Msigwa
Mei 14, 2014… Kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 17(1) na 8(2), Nafuta
umiliki wa vitalu vyote vilivyo chini ya Kampuni ya Green Miles Safaris
Ltd,” alisema Waziri Nyalandu. Alivitaja vitalu hivyo kuwa ni Lake
Natron GC East, Gonabis/ Kidunda- WMA na MKI- Selous.
“Hatua hii pia inafuta vibali vyote vya uwindaji
vilivyotolewa katika msimu huu wa uwindaji. Hii iwe onyo kwa kampuni za
uwindaji wa kitalii nchini kwa ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu za
uwindaji,” alisema Nyalandu.
Aliongeza, baada ya kupata tuhuma hizo aliiagiza
Idara ya Wanyamapori kufuatilia na kumhoji Mkurugenzi wa Kampuni ya
GreenMiles Safaris Ltd, ndipo walipobaini makosa ya kampuni hiyo.
Aliyataja makosa hayo yaliyokiuka Sheria ya
Wanyamapori namba 5 ya 2009 kuwa ni pamoja na wageni wa kampuni kuwinda
wanyama wasioruhusiwa wakiwemo nyani na ndege kinyume na kifungu cha 19
(1 na 2) na kuchezea watoto wa pundamilia na ngiri kinyume na kifungu
cha 19 (1).
“Kufukuza wanyamapori kwa magari na kisha kuwapiga risasi wakiwa ndani ya magari kinyume cha sheria,” alisema Nyalandu.
Akizungumzia hatua hiyo, Msigwa alisema ni ushahidi kuwa kambi ya upinzani bungeni inasema ukweli.