#DerevaMakini: Tujadili namna ya kupunguza ajali za mabasi ya abiria

Na Dotto Kahindi Nianze kwa kuwasalimu na kutoa shukran zangu kwa Blogu hii kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja yangu ambayo inalen... thumbnail 1 summary
Na Dotto Kahindi
Nianze kwa kuwasalimu na kutoa shukran zangu kwa Blogu hii kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja yangu ambayo inalenga kuishirikisha jamii katika kupata suluhisho la ajali za barabarani ambazo zimekuwa ni janga kubwa la kitaifa.

Mara kadhaa niliwahi kusikia takwimu za vifo vinavyotokana na magonjwa mbalimbali yakiwemo UKIMWI, Malaria, Vifo vya mama wajawazito n.k, na vifo hivi vilitia uchungu sana kwa jamii kiasi kampeni kadhaa zilianzishwa ili kupunguza vifo hivyo au kuvikomesha kabisa.

Jamii kwa kutambua athari zilizokuwa zikisababishwa na majanga hayo kijamii,  kiuchumi na kitaifa waliunga mkono kampeni hizo kwakuwa wao pia walikuwa wahanga wakuu na walipaswa kushiriki katika kubadili tabia na mienendo ili kuelekea kwenye Tanzania iliyo salama.

Nasikitika kutangaza kuwa Tanzania sasa kuna ugonjwa mpya unaitwa AJALI, kila siku ajali zinapoteza maisha ya wapendwa wetu. 

Takwimu zilizotolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dr. Harrison Mwakyembe mwisho wa wiki iliyopita zinaonyesha watu 1,126 wamepoteza maisha kwa ajali za barabarani kwa kipindi cha miezi mitatu, huku majeruhi ni 3,827 katika ajali 3,338.

Idadi hii ya ajali na vifo siyo ya kawaida, inatisha na kusikitisha sana ni wakati huu tunatakiwa kupambanua na kupata dawa ya kukabiliana na janga hili la ajali.

Tunaanzaje? Nani tuanze kumbana anayechangia ajali hizi? Ni maswali tunatakiwa kuyajibu kwanza kabla ya kuanza kutoa lawama, ni lazima tujue akina nani wanaohusika kwenye sekta hii ili tupate pa kuanzia kama tunataka kuziba ufa kwelikweli.

Mwakyembe ameunda kamati maalumu ya kutafuta chanzo na dawa ya ajali hizo, nimeona ni vyema kuunga mkono jitihada hizo kwa kuanzisha kampeni ya #DerevaMakini ambayo inalenga kuishirikisha jamii katika kukabiliana na ajali hizo ambazo zimekuwa mwiba kwa taifa. 

Kwa maoni yangu wafuatao ni wadau wa moja kwa moja wa sekta ya usafiri ambao wakitekeleza sawasawa majukumu yao ajali zitapungua; Askari wa Usalama Barabarani, Madereva, Abiria, Wamiliki wa vyombo vya usafiri, TRA, Sumatra, Bima, Vyombo vya habari, Tanroads, Miundombinu , NIT na vyuo vya namna hiyo, TBS, Wauzaji wa magari, mafuta na vipuli vya magari. 

Kupitia forum hii naomba kupata ushiriki wako mdau ili tutajadili kwa pamoja, toa maoni yako, ushauri na mapendekezo ukizingatia wadau waliotajwa hapo juu, maoni yako tutayatumia kwenye mada ifuatayo ambayo itakwenda kuchambua majukumu ya mdau mmoja mmoja.

Hii ni Kampeni ya Usalama barabarani yenye lengo la kupunguza ajali za barabarani ikilenga hasa mabasi ya abiria na imewezeshwa na Michuzi Blog, Tabianchi Blog na Transevents Marketing Limited.

Makala haya yatakuwa yakikujia kila wiki, kwa taarifa zaidi tembelea ukurasa wetu wa facebook