Tume "Operesheni Tokomeza" kutembelea Kigoma, Katavi, Rukwa na Mbeya

Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili imetangaza ratiba ya kwanza ya ziara yake katika Mikoa ya Kigoma, Katavi, Ru... thumbnail 1 summary
Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili imetangaza ratiba ya kwanza ya ziara yake katika Mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Mbeya ili kukusanya taarifa na kupokea malalamiko yaliyotokana na utekelezaji hiyo.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume hiyo iliyotolewa leo, Jumatano (Septemba 10, 2014) na Katibu wa Tume Wakili Fredrick Manyanda (pichani), ziara hiyo itaanza tarehe 17 mwezi huu na kumalizika tarehe 6 mwezi ujao.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Tume itakuwa katika mkoa wa Kigoma kuanzia tarehe 17 hadi 24 Septemba mwaka huu na kutembelea wilaya za Kigoma (tarehe 17 Septemba); Kibondo (tarehe 18 na 19), Kasulu (tarehe 20 na 22) na kumalizia Wilaya ya Uvinza tarehe 23 na 24.

Katika taarifa yake, Wakili Manyanda ameongeza kuwa Tume itakuwa Mkoani Katavi kuanzia tarehe 25 hadi 27 Septemba mwaka huu na ikiwa mkoani humo itatembelea wilaya ya Mpanda. Kati ya tarehe 28 na 30 Septemba, Tume itakuwa Mkoani Rukwa na itatembelea wilaya ya Sumbawanga.

Kwa mujibu wa Katibu wa Tume, kuanzia tarehe 1 Oktoba mwaka huu, Tume itakuwa mkoani Mbeya na itatembelea wilaya za Mbozi ( Oktoba 1 na 2); Mbeya (Oktoba 3) na Mbarali Oktoba 5 na 6.

Aidha, pamoja na mikutano hiyo, Wakili Manyanda amewaomba wananchi kutuma taarifa na malalamiko kwa njia ya barua, simu na barua pepe. Wananchi wanaweza kutuma barua kwa Katibu wa Tume, Tume ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili, SLP 9050, Dar es Salaam na barua pepe kwenda opereshenitokomeza@agctz.go.tz.

Kuhusu ujumbe mfupi wa maandishi, wananchi wanaweza kutuma kwa namba za simu: Tigo: 0714 826826; Vodacom: 0767 826826; Airtel: 0787 826826; na Zantel: 0773 826826.