Serikali
imekamilisha ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mpanda, mkoa wa
Katavi na hivyo kuufanya uwe wa kiwango kizuri tayari kwa kutumika kwa
ndege za binafsi na biashara.
Meneja
wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Bw Seneti Lyatuu alisema uwanja huo
umeboreshwa na hivyo, unaweza kutumika kutua na kuruka ndege za kiwango
cha kati na hata zile ndege kubwa zinaweza kutua kwa dharura.
Aliiambia
timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoa Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango iliyotembelea uwanja huo mwishoni mwa wiki kuwa uwanja huo
umeongeza idadi ya wasafiri mara dufu kutokana na ukarabati na upanuzi
uliofanyika.
Meneja wa Uwanja huo alisema idadi ya abiria imeongezeka kutoka abiria 285 mwaka 2009 hadi 2,390 mwaka 2013/14.
Bw.
Lyatuu alisema kuwa uwanja huo umekarabatiwa na barabara ya kuruka na
kutua ndege imerefushwa kwa kiwango cha lami kutoka urefu wa mita 1,500
na upana wa mita 30 hadi kufikia urefu wa mita 1,820 na upana wa mita
30.
Alisema
maeneo mengine yaliyokarabatiwa ni pamoja na kujenga uzio na mifereji
ya kupitishia maji ya mvua.
“Kwa sasa kiwanja kipo vizuri na ndege za aina zote zinaweza kutua hapa
uwanjani hivyo, tunawakaribishwa wadau wote kuutumia uwanja huu” alisema
Bw Lyatuu.
Eng.
Caroline Mntambo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Makao Makuu Dar es
Salaam alisema kuwa tayari wamealika mashirika ya ndege yanayofanya
biashara hapa nchini kuanzisha safari katika uwanja huo. Mashirika hayo
ni pamoja na ATC, Precision Air, Fast jet nk.
Eng
Mntambo alisema kwa sasa shirika la ndege la Auric Air tayari
limeanzisha safari za kwenda Mpanda ambapo linasafirisha abiria kutoka
Dar- Mpanda – Mwanza mara tatu kwa wiki.
Alisema ndege zingine zinazotua uwanjani hapo kwa sasa ni pamoja na za UNHCR, ndege za kukodi na ndege za serikali.
Meneja
wa Uwanja wa ndege wa Mpanda, Mkoa wa Katavi Seneti Lyatuu akiwaonesha
timu ya ukaguzi wa miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mpanda. Nyuma yake (mwenye suti
nyeusi) ni Mhandisi Caroline Mntambo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya
Ndenge Tanzania, Makao Makuu, Dar es Salaam.
Meneja
wa Uwanja wa Ndege wa Mpanda Bw. Seneti Lyatuu akifafanua jambo
wakati timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume
ya Mipango walipotembelea kiwanja hicho.
Timu ya ukaguzi ikitazama barabara ya kutua na kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Mpanda.
Barabara ya kutua na kurukia ndege katika uwanja wa ndege wa Mpanda, mkoani Katavi.
Mhandisi
Caroline Mntambo (mwenye suti nyeusi) akifafanua jambo kwa timu ya
wakaguzi kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. Uwanja wa ndege wa
Mpanda umekarabatiwa na kupanuliwa hivyo , kuwa katika hali nzuri kwa
matumizi ya ndege zote za binafsi na biashara.
PICHA NA JOYCE MKINGA