ForumCC ni Jukwaa la asasi zisizo za kiraia Tanzania
zinazojuhusisha na Mabadiliko ya Tabianchi. ForumCC inafanya shughuli zake
kuanzia ngazi ya chini kwa wananchi hadi kitaifa. Kwa lugha rahisi ambayo
mwananchi wa kawaida kabisa anaweza kuelewa.
Mabadiliko ya Tabianchi ni
mabadiliko ya muda mrefu na ya kudumu ya hali ya hewa, hasa jotoridi na mvua,
vile vile mabadiliko haya yanagusa kasi na mwelekeo wa pepo na mambo mengine
yanayohusiana na hali ya hewa. Moja ya athari za wazi wazi ni kuongezeka kwa
joto, pia kuongezeka sana au kupungua sana kwa mvua. Athari hizi tayari sisi
kama sehemu ya dunia tumezishuhudia katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Sasa
kwa hili la Buguruni kwa Mnyamani nalo lina sura yake ambayo haikuwekwa wazi na
watoa taarifa kwa umma hasa kilichosababisha.
Mnamo tarehe 22 march 2015 saa tisa mchana Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua kubwa katika ukanda
wa pwani itakayonyesha kwa siku tatu mfulilizo. Unakanda huu unajumuisha mikoa
ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na
Pemba. Mamlaka hiyo ilitoa tahadhari ya ongezeko la mvua kwa zaidi ya milimita
50 ndani ya saa 24.
Masaa machache baada ya tahadhari kutolewa mvua ilianza
kunyesha katika maeneo mengi, ikiwemo
Dar es Salaam, mvua ambayo ilipelekea maafa makubwa kwa wakazi zaidi ya 5,170
katika eneo la Buguruni kwa Mnyamani. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya
Mtaa Bw Abdallah Mng’ae anasema takribani nyumba 517 zilihadhiriwa na mvua
kubwa iliyonyesha na kila nyumba ina wastani wa wakazi 10.
Nini Sababu za
Mafuriko Katika eneo la Buguruni Kwa Mnyamani?.
Sababu iliyotolewa kwa vyombo vya habari kama kisababishi
cha mafuriko hayo ni kuziba kwa mfereji wa kupitishia maji katika eneo hilo,
ambapo chanzo chake ni wizi wa chujio la kuchuja takataka. Inasemekana chujio
hilo liliibiwa na kuuzwa kama chuma chakavu, biashara ambayo imesababisha
kuhujumiwa kwa miundombinu mbalimbali ya maendeleo katika maeneo mengi hapa
nchini.
ForumCC inapinga na kukemea kwa nguvu zote wizi wa namna
hiyo ambao unarudisha nyuma maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Pia tunatoa
wito kwa jamii kulinda miundombinu na kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika
pale wanapobaini watu wanaohujumu miundombinu mbalimbali. Wizi ni kitendo
kisichokubalika, na jamii isikae kimya pale inapobaini wezi hawa, ni vizuri
taarifa zikatolewa kwa vyombo husika ili hatua za kisheria ziweze kuchukua
mkondo wake.
Jicho la Tatu Kuhusu
Mafuriko
Kwa kutumia jicho la tatu utagundua kuwa kuibiwa kwa chujio
kwenye mfereji unaopitisha maji katika eneo la Buguruni kwa Mnyamani si
kisababishi pekee cha mafuriko hayo. Kuna visababishi vingine vyenye uzito sana
ambavyo havikuzungumziwa kabisa. Kuna maswali kadha wa kadha ya kujiuliza
kuhusu janga hili lililowakumba wakazi wa Buguruni kwa Mnyamani.
·
Je ongezeko la mvua kwa milimita 50 si sababu
mojawapo ya mafuriko kutokea?.
·
Je ukubwa wa mfereji wa kupitishia maji katika
eneo la tukio unaweza kuhimili ongezeko kubwa la maji?.
·
Je hilo chujio lingeweza kuhimili uchafu mwingi
ambao ungetokana na ongezeko la mvua?.
·
Je kuna watu ambao huondoa uchafu kwenye
machujio haya wakati mvua ikinyesha ili kudhibiti lisizibe?.
Majibu ya maswali haya moja kwa moja yanaonyesha uwezekano
mkubwa sana wa mafuriko kutokea hata kama chujio lililoibiwa lingekuwepo. ForumCC
inaona hivyo kwa sababu ni ukweli usiopingika kuwa uwezo wa miundombinu yetu
kuhimili mafuriko bado upo chini sana. Na kutokana na uwepo wa mabadiliko ya
tabianchi, ongezeko la mvua kupita kiasi kwa muda mfupi ni moja ya vitu ambavyo
vitakuwa vinajirudia hivyo basi tusipojenga miundombinu imara na yenye
kuzingatia uwepo wa mabadiliko ya tabianchi tutazidi kuathirika zaidi.
Kulingana na mazingira ya mfereji wa kupitishia maji katika
eneo la Buguruni kwa Mnyamani na mpango wa makazi ni dhahiri kuwa hata chujio
lingekuwepo mafuriko yangetokea tu.
Ni wakati sasa wa wananchi kuhimiza serikali yao ijenge
miundombinu bora ambayo inazingatia uwepo wa majanga tofauti tofauti katika jamii
yetu. Wakati huo huo wananchi nao wanawajibu wa kuboresha makazi yao kulingana
na mabadiliko ya tabianchi.
Ni wito wetu kwa watoa taarifa za majanga mbalimbali na
masuala mengine kueleza kwa kina kuhusu tukio ili jamii ijue ukweli na pale
ambapo inaweza kushiriki kuboresha, kuepuka au kuhimili wajue wajibu wao.
Vilevile maelezo ya kina na ya jicho la tatu yatakuwa ni elimu tosha kwa jamii
na wadau wengine.
Tuboreshe miundombinu na Kuilinda