Wito huo umetolewa na afisa mazingira wa wilaya ya Bagamoyo
Shedrack Maximilian wakati wa zoezi la upandaji miti katika shule ya sekondari
Bagamoyo mkoani Pwani , kulikofanywa na
asasi zisizo za kiserikali na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za jijini Dar
es salaam na wenyeji shule ya sekondari Bagamoyo jumamosi wiki hii.
Afisa huyo aliyekuwa akimwakilisha mkuu wa wilaya ya Bagamoyo
amesema watanzania wanakila sababu ya
kupanda miti na kuhifadhi mazingira ili kuendelea kuibakisha nchi katika kijani
kibichi. Amesema sababu za kiuchumi ,
umaskini na kibiashara zisiwe chanzo cha uharibifu wa mazingira na kukata miti
hovyo.
“kama sisi hapa Bagamoyo tupo karibu na jiji la Dar es
salaam lenye mahitaji ya matumizi ya kuni na mkaa. tusipopanda miti kutabaki jangwa, hatutaki kuruhusu hili kutokea
maana hatujui dunia inaisha lini . kuna
vizazi vinazaliwa hamna mahali pengine
watapata miti na kuwa na mazingira bora”amesema Shadrack
Naye mwakilishi wa shirika la Norwegian church Agoustina Mosha amesema shirika lao ni mfadhili wa miradi
mbalimbali ya maendeleo ya vijana, wajasiliamali na miradi ya kupambana na
mabadiliko ya tabianchi.
“shirika letu limeanza toka mwaka 2011 hapa nchini, tunafanya
shughuli zetu na asasi za kiraia na kidini kama Bakwata, Tec ,Katholiki , Buddha
na Hindu. Tumefikia wilaya zaidi ya 60 nchi nzima, tunapenda kufanya kazi na
vijana kwa sababu ndio wapo wengi nchini kwa mujibu ya sensa ya watu na makazi
ya mwaka 2012, ukiwakusanya vijana na kuwapa mafunzo ni rahisi kuchukua hatua
kutokana na kuwa kundi kubwa”amesema mama Mosha.
Akitoa shukrani kwa ugeni huo mkuu wa shule ya Bagamoyo Halfani Milongo amesema wamepokea zawadi ya
miti kwa mikono miwili na watajitahidi
kuilinda na kuitunza ili isiweze kukauka na kufa.
“tuna vijana wapenda
mazingira na wapo tayari kuitunza kwa nguvu zao zote, sote tunajua umuhimu wa
miti katika kupunguza hali joto , tutashirikiana na vijana wetu na tuna ahidi baada ya miaka kadhaa karibuni kuja kujionea miti mliyotuletea hapa shuleni
ikiwa imestawi vyema” anamaliza Mwalimu huyo.
Naye kiongozi wa Tanzania Youth Network Agnes Mgongo ambao walikuwa washiriki katika uzinduzi huo wa upandaji miti, amesema wameshiriki zoezi hilo kwa kutambua faida ya
miti kwa ustawi wa jamii na utunzaji mazingira.
Pia ni jukwaa ambalo kama vijana wamepata kukutana na vijana wengine
kutoka sehemu mbalimbali na kubadilishana mawazo na uzoefu juu ya
maswala ya vijana.
“vijana wengi wa
kitanzania tupo hatutumii fursa zinazopatikana ndani na nje ya nchi , tofauti na vijana
wenzetu wa Afrika Mashariki. Ni wakati
wetu sasa kubadilika na kwenda na wakati kwa kuchangamkia fursa zinazojitokeza
mahali popote dunia, tumepewa akili na maarifa tusisubiri serikali itufanyie kilakitu vijana tunaweza” anamaliza kusema Agnes
Mgongo.
Uzinduzi huo ulikuwa sehemu ya kutoa elimu ya upandaji miti
kwa shule ya sekondari ya Bagamoyo na vijana kwa ujumla kulikofanywa na vijana kutoka asasi
mbalimbali za mazingira kutoka jijini Dar es salaam pamoja na chuo cha
mazingira cha Institute of Environment Climate and Development Sustainability kilichopo Bunju jijini Dar es salaam.