Imefahamika kuwa mimea mingi hasa mazao ya chakula inaandamwa na
magonjwa ya aina mbalimbali yanayoleta usumbufu mkubwa na kurudisha nyuma
kilimo pamoja na maendeleo kwa jumla
Waandishi wa habari na bloggers wakizungumza na mmoja wa wakulima wa mahindi, Alfred Mwasi
Changamoto hii unaweza kudhani inewakumba wakulima wa Tanzania pekee, la
hasha hili ni tatizo linalowakabili wakulima katika nchi nyingi za kiafrika.
Lakini swala la msingi la kujiuliza ni nini sababu ya kuongezeka kwa
magonjwa hayo. “Kadri mvua inapokosekana tunaona magonjwa ya mazao nayo
yanaongezeka na kuharibu mazao yetu” anasema Magret Mwasi mmoja wa wakulima
kutoka kwenye kijiji cha Kipuzi kwenye Kaunti ya Taita Taveta.
Mama huyu anakiri kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya kupungua kwa mavuno
ya zao la mahindi na athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini hakuna taarifa
za kutosha kuwasaidia wakulima hao kukabiliana na changamoto hizo
Taasisi ya ICIPE inafanya utafiti katika vilima vya Taita nchini Kenya chini
ya mradi wa CHIESA ambao unalenga kujua mabadiliko ya tabianchi yanavyoleta
athari katika kilimo hasa hasa zao la mahindi.
Mkuu wa mradi huo wa utafiti Paul-Andre Calatayud anasema magonjwa ya zao
la mahindi yameongezeka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na
kuathiri mfumo mzima wa kilimo na utekelezaji wake.
Anasema mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha mtawanyiko na wingi
wa wadudu waharibifu na hivyo kuharibu mazao ya nafaka mashambani na mavuno
yake.
“Utafiti wetu unalenga katika kupata suluhu ya kukabiliana na magonjwa
ya mahindi, akiwemo funza (stem borer) ambaye amekuwa ni mharibifu sana katika
zao la mahindi na baadae tutatoa majibu ya utafiti wetu ili uweze kutumiwa na
wakulima hawa” anasema Paul
Wakulima mahindi katika vijini vinavyozunguka vilima vya Taita wameweka
matumaini yao kwenye utafiti huo wakingoja kwa shauku kupata suluhu ya magonjwa
na mahindi ambayo yamekuwa mwiba mchungu kwao.
“Tuna matumaini makubwa na utafiti huu, tukiamini kwamba utakuja
kutukomboa kutoka kwenye shida hii ya kukosa mazao kila mwaka” anasema Nancy
Makio mmoja wa wakulima wa mahindi kutoka kijiji cha Mbengoni Kenya.
Magonjwa yanayoathiri mahindi ni mengi lakini mdudu funza ama bungua
amekuwa ni tishio kubwa kwa mahindi sio tu Kenya bali hata hapa nyumbani Tanzania,
hivyo kupatikana kwa njia ya kuangamiza mdudu huyo kutaleta tija kwa nchi zote
za Afrika Mashariki
Ripoti hii imewezeshwa na Tabianchi kwa kushirikiana CFI chini ya mradi
wa Medias21 2015, ikiwa ni juhudi za kutoa elimu ya mabadiliko ya tabianchi
kuelekea mkutano wa kimataifa wa mazingira COP21