Maoni: Ongezeko la tozo mafuta ya taa litachochea uharibifu wa mazingira na kuongeza umasikini kwa wanyonge

Hatua ya Serikali ya kupandisha maradufu tozo ya mafuta ya taa katika Bajeti ya 2015/16, imewaacha njia panda mamilioni ya wananchi masik... thumbnail 1 summary
Hatua ya Serikali ya kupandisha maradufu tozo ya mafuta ya taa katika Bajeti ya 2015/16, imewaacha njia panda mamilioni ya wananchi masikini, hasa waishio vijijini. 

Ni hatua ambayo inaonekana bayana kufifisha matumaini yao na kuwafanya wajione kama raia wa daraja la pili, kujiona wako nje kabisa ya vipaumbele vya Serikali katika mipango yake ya maendeleo. Kwa kipindi kirefu sasa, Serikali imekuwa ikipandisha tozo ya nishati hiyo kwa kisingizio kwamba inadhibiti uchakachuaji wa mafuta ya petroli na dizeli ambao umekuwa ukifanywa na kampuni na wafanyabiashara mbalimbali.
Akiwasilisha bajeti hiyo ya Sh22.5 trilioni bungeni mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya pia alitangaza nyongeza ya tozo ya petroli na dizeli, huku akisema tozo ya mafuta ya taa itapanda maradufu kutoka Sh100 hadi Sh150 ili kuwadhibiti wachakachuaji wa mafuta hayo.

Kama ilivyotarajiwa, wananchi wengi wameipokea hatua hiyo ya Serikali kwa mshtuko na ghadhabu kubwa, huku wasomi na wataalamu wa masuala ya uchumi wakisema bajeti hiyo ni kitanzi tosha kwa wananchi wote masikini.
Hoja yao, ambayo sisi tunadhani ni ya msingi ni kwamba kulikuwa na vyanzo vingine vya mapato badala ya kuongeza kodi katika mafuta ambayo itachochea mfumuko mkubwa wa bei ya bidhaa na huduma nyingine nyingi na kusababisha maumivu makubwa kwa wananchi. Kwa mfano, tunakubaliana nao wanaposema kwamba Serikali ingeweza kukusanya kodi nyingi kutoka kwa wamiliki wa majengo makubwa ya biashara, nyumba za kukodisha na kuishi. Moja ya vikwazo vikubwa ni kwamba wanasiasa na viongozi wakubwa serikalini ni miongoni mwa wamiliki wa nyumba hizo na vitega uchumi mbalimbali hapa nchini.
Tunapata shida kuelewa kwa nini inakuwa vigumu kwa Serikali kupanua wigo wa kodi badala ya kung’ang’ania ongezeko la tozo katika mafuta, hasa ya taa, wakati ikijua kwamba mafuta ya taa ni nishati pekee kwa wananchi wengi waishio vijijini. Kwa sababu hiyo, umasikini vijijini unazidi kukua, ikiwa ni pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na ukataji wa miti kama nishati pekee. Pamoja na kuanzishwa kwa Kamati ya Bunge ya Bajeti ili isaidie kuibua vyanzo vipya vya mapato, bado iliona ni busara kutoongeza tozo kwenye bia, lakini ikaona ni murua kuongeza tozo kwenye mafuta ya taa, dizeli na petroli.
Pamoja na ongezeko hilo kuwekwa ili kuwabana wachakachuaji wa mafuta, inashangaza kuona Serikali imeshindwa kuwakamata wachakachuaji hao ingawa wanajulikana kwa majina na sehemu wanazochakachulia mafuta hayo. 

Litakuwa jambo la kushangaza iwapo vyombo vya usalama kwa miaka nenda rudi ambayo uhalifu huo umekuwa ukiendelea, vitakuwa vimeshindwa kuwabaini wahalifu hao na kuwachukulia hatua stahiki. Badala yake, Serikali imeona ni bora zaidi kuwaadhibu wananchi zaidi ya milioni 30 waishio vijijini badala ya kuwakamata na kuwaadhibu watu wasiozidi 200 ambao wanachakachua mafuta. 

Kwa muda mrefu sasa zimekuwapo tuhuma kwamba wengi wa wachakachuaji wa mafuta, ni wafadhili wakubwa wa baadhi ya wanasiasa na viongozi serikalini.
Hakuna asiyejua kwamba nishati ya mafuta ya taa ni mkombozi pekee wa wananchi katika maeneo ya vijijini. Hivyo, kupandisha tozo ya nishati hiyo maradufu ni kuwanyonga. Tutawashangaa wabunge iwapo wataipitisha tozo hiyo pamoja na zile zinazohusu dizeli na petroli.

Chanzo: MCL