TPA kuwawezesha waandishi wa habari wanaoandika habari za kukomesha ujangili

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa shilingi milioni mbili kwa Taasisi ya Ha... thumbnail 1 summary
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetoa msaada wa shilingi milioni mbili kwa Taasisi ya Habari Development Association kwa ajili kuandaa mafunzo ya kuwawezesha waandishi wa habari kujenga weledi wa kufanya tafiti na kuandika habari za kupambana na ujangili.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Awadh Massawe alikabidhi hundi ya thamani ya fedha hizo kwa Mkurugeni wa taasisi hiyo, Bw. Kunze Mswanyama jana jijini Dar es Salaam.

“Tunaunga mkono juhudi hizi za kupambana na ujangili,” alisema Bw. Massawe mjini hapa.
Alisema TPA imefanya hivyo kwa kuwa nchi ina tatizo la uwindaji haramu hasa wa ndovu na usafirishaji wa pembe za ndovu na kulisababishia hasara taifa kupitia mipaka ya taifa.

Alifafanua kwamba bandari ya Dar es Salaam ni sehemu ya mpaka wa taifa, hivyo lazima TPA iunge mkono juhudi za kuelimisha jamii na kuzuia uhalifu huo.

“Tunazidi kuimarisha ulinzi katika bandari kwa kuwa ni sehemu ambayo bidhaa haramu zinaweza kupitishwa,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa sasa wanatarajia kufunga kamera 400 za CCTV ili kuimarisha na kuwa skana tatu zimeletwa banadarini kwa ajili yakuziongezea nguvu skana mbili zilizopo.

Pia alisema wanatarajia kupata msaada wa mbwa maalumu wa ulinzi watakaotolewa na serikali ya Marekani. 

Alisema TPA inaendelea kuwajengea uwezo wafanyakazi kimaadili ili kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uaminifu kwa faida ya taifa.

Mkurugenzi wa Habari Development Association, Bw. Mswanyama alisema fedha walizopewa watazitumia kwa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari 54 wa maswala ya ujangili kupata weledi na kutafiti na kufichua ujangili.

“Tunahitaji kujenga weledi zaidi wa kupambana na ujangili wa rasirimali zetu ili taifa liweze kunufaika nazo,” alieleza.

Alisema taasisi yao inaundwa na waandishi wa habari wanaoandika habari za kupambana na ujangili na rasirimali nyingine katika mbunga mbalimbali zikiwemo za Sadani, Serengeti, Mikumi na Selou.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), Bw. Awadhi Massawe katikati akizungumza wakati alipokuwa akikabidhi hundi ya shilingi milioni mbili(2m/-) kwa Taasisi ya Habari Development Association, kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo  waandishi wa habari kufanya tafiti na kuandika habari za kupambana na ujangili nchini. Taasisi hiyo inaundwa na waandishi wa habari wanaoandika habari za ujangili kwa kina. Kulia ni Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bw. Kunze Mswanyama na kushoto ni Ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa TPA, Bw. Focus Mauki
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), Bw. Awadhi Massawe kushoto akimkabidhi hundi ya shilingi milioni mbili (2m/-) Mkurugeni wa Taasisi ya Habari Development Association, Bw. Kunze Mswanyama kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kufanya tafiti na kuandika habari za kupambana na ujangili. Taasisi hiyo inaundwa na waandishi wa habari wanaoandika habari za ujangili kwa kina.