Dotto Kahindi
RoadToParis2015 with tabianchiblog&CFIMedias21
RoadToParis2015 with tabianchiblog&CFIMedias21
Wanahabari ni miongoni mwa watu wenye nguvu kubwa ya
ushawishi ambao wamekuwa wakitumika kama daraja kati ya vikundi tofauti hasa
katika kupasha habari.
Mawasiliano kati ya viongozi, wanasayansi, watafiti na
wananchi katika jamii mbalimbali yamekuwa yakiwezeshwa kwa kiasi kikubwa na
vyombo vya habari na waandishi wa habari wenyewe.
Waandishi wameonekana kuwa muhimu sana katika maendeleo na
ustawi wa mataifa mbalimbali kutokana na kuyachambua mambo magumu, kuyalainisha
na kuyafikisha kwa wananchi ili waweze kuyaelewa kwa urahisi.
Hata hivyo waandishi wengi wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo
kukosa uelewa na ufahamu wa kutosha wa kuandika habari za sayansi na mazingira,
jambo ambalo linafanya habari nyingi za aina hiyo kukosa ladha ya kuwavutia
wasomaji.
Kwa kipindi kirefu kumekuwa na utengano baina ya waandishi na
wanasayansi, jambo ambalo limepelekea jamii kukosa kupata habari za kina zenye
majawabu ya matatizo yanayohusiana na sayansi.
Hii ni kutokana na wanasayansi wengi kutoa ripoti zao katika lugha ngumu
yenye kuwatatiza waandishi wa habari ambao ndio wawasilishaji wa mwisho wa
taarifa hizo kwa wananchi.
Mkutano wa wanasayansi mjini Paris, Ufaransa, Picha na Christophe Maitre INRA |
Wanasayansi wamefikia mahala wamegundua kuwa kazi zao haziwezi kuwa na
maana kama hazijalainishwa na kuwa katika hali nzuri ya kumezwa na walaji wa mwisho
na ndio maana wameona umuhimu wa kushirikiana na waandishi wa habari ili kazi
zao ziwafikie wananchi
“Tungependa kuimarisha ushirikiano wetu wanasayansi na waandishi wa
habari, kuanzia katika hatua za mwanzo mpaka mwisho katika shughuli zetu za
utafiti, hii itawezesha taarifa zetu za kisayansi kuwafikia wananchi kwa
urahisi na katika lugha nyepesi” anasema Madaka Tumbo, mtafiti kutoka
kwenye Taasisi
ya Kutathimini Rasilimali Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (IRA)
Katika kuhakikisha kuwa waandishi
wa habari hasa wa kizazi kipya wanakuwa na uwezo wa kuripoti habari za
mazingira, Shirika la Habari la Ufaransa (CFI) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa
la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO wametoa mafunzo kwa
waandishi wa habari kutoka Tanzania, Kenya na Madagascar.
Mafunzo hayo yanalenga kujengea
uwezo wa waandishi hao kuripoti habari za sayansi na mazingira kwa kushiriki
kwenye mikutano ya wanasayansi ili kujifunza kwa vitendo namna ya kuandaa na
kuandika habari za namna hiyo
Ikiwa kama nchi mwenyeji wa mkutano
wa mazingira, Urasansa kupitia shirika la habari za Ufaransa (CFI), french
media cooperation agency) kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya
Ufaransa wameanzisha mradi wa mafunzo ya uandishi wa habari na mabadiliko ya
tabianchi (Media21 Journalism and Climate Change)
Lengo la
mradi huo ni kuwajengea uelewa wa mambo mbalimbali wakati wa mkutano wa
mazingira, kuwezesha uelewa kwa wananchi juu ya mabadiliko ya tabianchi na
kuwawezesha waandishi wa habari juu ya namna ya kuwasilisha kazi zao katika
lugha inayoeleweka kwa wasomaji wao.
Akiwa katika chakula cha pamoja na
waandishi wa habari kutoka kutoka Tanzania, Kenya na Madagascar Mkurugenzi Mkuu wa CFI, Etienne
Fiatte anabainisha kuwa “Hii ni sehemu
ya mpango wetu wa kushirikiana na vyombo vya habari Barani Afrika katika
kuchangia upashaji habari za mabadiliko ya tabianchi tukielekea kwenye mkutano
wa wanachama wa mabadiliko ya tabianchi COP21 desemba mwaka huu, tunamatumaini
makubwa kwa waandishi hawa kwamba watajifunza na kutoa matokeo chanya katika
mradi huu”
Waandishi
wa habari kutoka nchi hizo tatu awali walikutana mjini Nairobi nchini Kenya
kupata mafunzo ya namna ya kuandika habari za sayansi na mabadiliko ya
tabianchi kwa lugha tamu na ya kuvutia kwa wasomaji kabla ya kushiriki kwenye
mkutano wa wanasayansi unaofanyika mjini Paris Ufaransa.
“Mafunzo
haya yamenipa uwezo wa kuandika habari za mabadiliko ya tabianchi katika lugha
nyepesi, naweza kuzichanganua taarifa ngumu za kisayansi katika makundi madogo
madogo yanayoweza kueleweka moja kwa moja kwa wasomaji wa habari zangu” anasema
Sophia Mbuguah mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka Kenya na kuongeza
kuwa: “Hapo awali niliandika habari zangu kwa ujumla sana na ilikuwa ngumu kwa
msomaji kuguswa na habari hiyo, lakini sasa naweza kuhusianisha habari yangu na
mambo mtambuka kama uchumi, kilimo, afya na kutoa uchambuzi wa kina unaomfanya
msomaji aelewe kwa urahisi”