Wanasayansi wakutana kufyeka njia ya kuelekea makubaliano ya mkataba mpya wa mazingira wakati wa COP21

RoadToParis with tabianchiblog&CFIMedias21 Waswahili husema usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Umuhimu wa nuru katika giza ni s... thumbnail 1 summary
RoadToParis with tabianchiblog&CFIMedias21

Waswahili husema usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Umuhimu wa nuru katika giza ni sawa sawa na umuhimu wa tafiti za wanasayansi katika kupata ufahamu na uvumbuzi wa mambo mbalimbali katika jamii.

Wanasayansi wamekuwa na mchango mkubwa sana katika kutafiti na kuibua majawabu ya mambo mbalimbali ambayo jamii ya watu imekuwa haina ufahamu nayo.

Sehemu ya wanasayansi wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa siku Julai 7, 2015 (Picha na tabianchi blog)
Julai 7, 2015 wanasayansi zaidi ya 2000 kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni wamekutana kwenye mkutano wa wanasayansi (Our Common Future Under Climate Change) mjini Paris, Ufaransa kwa lengo la kutoa tathmini ya hali ya mabadiliko ya tabianchi.

Malengo mengine ni pamoja na kutafuta njia za kukabliana na mabadiliko ya tabianchi kama njia ya kuelekea kwenye kufikia makubaliano ya mkataba mpya wa mazingira hapo desemba mwaka huu wakati wa Mkutano wa ishirini na moja wa nchi wanachama wa Mabadiliko ya Tabianchi COP21.

Wanasayansi hawa wanajadili na kupima ushahidi wa mabadiliko ya tabianchi ambao umekuwa ukitolewa kupitia tafiti mbalimbali ili kutoa fursa kwa jamii kujua na kujadili mambo ya kisayansi yanayogusa maisha yao.

Mkutano huo ambao unafanyika kipindi kifupi baada ya ripoti ya tano (AR5), ya jopo la kimataifa kuhusu Mabadiliko ya tabianchi (IPCC), pia utatoa nafasi kwa wadau na wanasayansi kujadili majawabu ya namna ya kupunguza na kuzuia mabadiliko ya tabianchi. 

Maeneo ambayo yanajadiliwa ni pamoja na elimu ya maendeleo endelevu, sayansi, sera na jamii, mambo ya bahari na hali ya hewa, maji salama na elimu ama ufahamu kwa watu wa maeneo ya vijijini.

Mkutano huo umeandaliwa chini ya mwamvuli wa ICSU, Future Earth, UNESCO, taasisi za utafiti za Ufaransa na kufadhiliwa na serikali ya Ufaransa.