Dotto
Kahindi
RoadToParis2015 with Tabianchiblog&CFIMedias21
Wakazi katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria
huenda wakakumbwa na hatari ya kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa
kunyesha katika maeneo hayo na ziwa hilo kufurika maji, imefahamika.
Ziwa Victoria |
Utafiti
uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa katika miaka 10 ijayo kutakuwa na
ongezeko kubwa la mvua katika maeneo yote yanayozunguka Ziwa Victoria ikiwa ni
pamoja na nchi jirani za Kenya na Uganda.
Utafiti
uliofanywa na Idara ya Sayansi ya Majini, Nchi kavu na Anga katika Chuo cha
North Carolina State cha nchini Marekani, unatoa tahadhari kwa wananchi na
mamlaka mbalimbali za serikali na binafsi kuzingatia utafiti huo wakati wa
kuandaa mipango yao ya kimaendeleo na kiuchumi kwani utaleta madhara makubwa.
Mkurugenzi
wa Idara hiyo Dr. Fredrick Semazzi anasema miongoni mwa madhara
yatakayojitokeza kutokana na ongezeko la mvua hizo ni pamoja uharabifu wa
miundombinu ya barabara, reli, makazi, vitega uchumi na miundombinu ya
uzalishaji wa umeme.
Wakati
hali ikitarajiwa kuwa hivyo kwenye ziwa victoria maeneo ya kaskazini mwa
Tanzania, kwenye mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro itakumbwa na ukame
mkali.
Dr. Semazzi |
Akiwasilisha
mada kwenye Mkutano wa tano wa Mabadiliko ya Tabianchi kwa Afrika (CCDA-V)
uliofanyika Victoria Falls Zimbabwe, Semazzi anasema ili kukabiliana na janga
hilo ni vyema mamlaka za mipango miji kuweka mipango ya kukabiliana na jambo
hilo ambalo linatajwa kutokea kati ya miaka 10 hadi 15 kuanzia sasa.
“Ongezeko
la mvua kwenye ukanda wa ziwa Victoria linatarajiwa kuwa kubwa baada ya miaka
kumi kuanzia sasa, ukiiangalia unaiona ni miaka mingi lakini kimipango na
maendelea ni michache sana, hivyo malmaka husika zinapaswa kulizingatia hilo
katika kuweka mipango yao” anasema Semazzi
Utafiti
huo pia umeonyesha kuwa kufurika kwa maji kwenye ziwa victoria kutasababisha
uharibifu kwenye uzalishaji kupitia kilimo, ufugaji na uvuvi.
Pengine
utafiti huu umetolewa wakati muafaka ambapo kumekuwa na kasi ya uwekezaji katika
jiji la Mwanza na maeneo yanayolizunguka ikiwemo ujenzi wa hoteli, majengo
makubwa ya biashara (malls) na viwanda ambavyo bila tahadhali vinaweza kukumbwa
na janga hilo.
Kwa
takribani miaka 30 sasa kiwango cha mvua kwenye ukanda wa ziwa victoria
kimeendelea kupungua hali ambayo inatajwa kusababishwa na mabadiliko ya
tabianchi lakini hali hiyo inatarajiwa kuwa tofauti katika miaka kumi ijayo kwa
kiwango hicho kuongezeka kwa haraka katika ukanda huo.
Ziwa Victoria
Ziwa
Victoria lililopo Kanda ya Ziwa ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya maendeleo ya
Tanzania, na hata nchi nyingine kama vile Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya na
Misri inayopata huduma ya maji ya Mto Nile unaoanzia kwenye ziwa hili la kwanza
kwa ukubwa barani Afrika na la pili kwa ukubwa duniani.
Kutokana na
kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira katika ziwa hilo lenye eneo la ukubwa wa
kilometa za mraba zaidi ya 68,100, utafiti wa kitaalamu unathibitisha kwamba
samaki wamepungua kutoka kati ya tani 400,000 na 500,000 hadi tani 243,564 kwa
mwaka 2010, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.
Ziwa
Victoria lenye kina cha wastani wa mita 40 (futi 130), na mwambao wa urefu wa
mita 4,828 (maili 3,000) linapata
maji yake mengi kutokana na mvua (80%) na kutoka vijito vingi vidogo. Mto mkubwa
unaoingia Victoria ni Mto unaotiririka kutoka upande wa magharibi.
Eneo la maji ya ziwa imegawanywa kwa
6% (4,100 km2) nchini Kenya, 45% (31,000 km2) nchini Uganda, na 49% (33,700
km2) nchini Tanzania ambapo miji mikubwa kandokando ya ziwa hilo ni Jinja na
Entebe kwa Uganda, Kisumu kwa Kenya na Mwanza kwa Tanzania.
Eneo la kijiografia lilipo Jiji
la Mwanza kunalifanya kuwa jiji pekee kubwa katika Ukanda wa Ziwa Victoria
linalofikika kirahisi kutoka nchi zote tano zinazounda Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), za Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya na Tanzania.
Vitega uchumi vya kimkakati kama
ilivyo Rocky City Mall, vinalipa Jiji la Mwanza fursa kubwa zaidi kuweza
kuiishi ndoto yake ya kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Maziwa Makuu.
Rock City Mall. Picha na Milardayo.com |
Lakini wataalamu wa mambo ya hali
ya hewa na mipango miji wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa ya madhara
yanayoweza kujitokeza kutokana na kufurika kwa ziwa Victoria kama utafiti huu
unavyoonyesha.
Hatua madhubuti
Dr.
Semazzi anashauri ushirikishwaji wa wanasayansi ili wafanye utafiti kabla ya uandaaji
wa mipango yeyote ya maendeleo ile ili kuweza kubaini madhara yanayoweza
kujitokeza katika kipindi hicho.
“Mamlaka
zinahitaji kupata mpango mzuri utakaoweza kubainisha madhara na ujio wa janga
hilo mapema ili kuwe na muda wa kutosha kupanga namna ya kukabiliana nayo”
anasema Semazzi
Anasema
nyenzo zinazotumika kupima hali ya hewa hazitasaidia kitu kama hakutatolewa mafunzo
kwa wataalamu wa hali ya hewa, maafisa mipango miji na wanasayansi ili
kuwajengea uwezo wa kubaini mambo hayo kabla ya kupanga mipango ya muda mfupi
au mrefu.
“Sijui
kama wanasayansi wanashirikishwa kikamilifu katika mipango ya maendeleo, lakini
itakuwa vizuri kuwashirikisha vinginevyo itakuwa ni uharibifu wa fedha watu kuwekeza
katika miradi ambayo itaharibika kwa muda mfupi” anasema Semazzi na kuongeza:
“Watu
wanatakiwa kuwa makini na suluhu za muda mfupi kwa kuwa huongeza madhara zaidi
nadhani ni muhimu kuishirikisha jamii kuanzia ngazi za chini mpaka ngazi za juu
ili kupeana ufahamu wa kutosha juu ya mambo haya”.
Tayari kumekuwepo na jitihada za
kupunguza athari za kimazingira kwenye ziwa Victoria ambapo Mradi wa Uhifadhi
wa Mazingira wa Bonde la Ziwa Victoria (LVEMP II) umekua mkombozi mkubwa wa
mazingira kwa wananchi wa ukanda wa Ziwa, ikiwa pamoja na kudhibiti tatizo la
magugu maji.
Akizungumza jijini Mwanza katika
maonyesho ya kuadhimisha siku ya Mazingira Dunia, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais-Mazingira Mhe. Binilith Mahenge anasema mradi huo ambao
unasimamiwa na kuratibiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) mpaka
sasa kwa upande wa Tanzania miradi midogo iloyochini ya mradi wa LVEMP II
ipatayo 19 imekamilika na 197 iko katika hatua za utekelezaji.
Pengine utafiti huu utakuwa
chachu kwa kamisheni hii kufikiria juu ya kukabaliana na mafuriko
yatakayojitokeza hapo usoni kwa mujimu wa utafiti huo ambao ni muhimu
kuzingatiwa na kufanyiwa kazi mapema.
Hotuba ya aliyekuwa Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi katika serikali ya awamu ya nne, Dk. Titus Kamani,
aliyoiwakilisha bungeni wakati wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa
mwaka 2014/2015 inaeleza jumla ya tani 38,574 za
mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 44,260
zimeuzwa na kuiingizia Serikali mapato ya shilingi bilioni 6.1.
Pamoja na kwamba idadi hiyo ya samaki waliouzwa na
kiwango cha fedha kilichopatikana sio cha samaki waliovuliwa ziwa Victoria
pekee lakini inatoa mwanga wa kaisi gani sekta ya uvuvi nchini inavyochangia pato
la mwananchi na taifa kwa ujuma na kwamba kufurika kwa ziwa Victoria kunaweza
kuathiri uchumi huo
Habari hii imefadhiliwa na CFIMedia21 Project