Dotto Kahindi,
Le Bourget, Paris, Ufaransa
Mahitaji Matatu kwa nchi zinazoendelea |
Majadiliano yanayoendelea kwenye Mkutano wa
Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Mjini Paris, Ufaransa huenda yakashindwa
kuzaa matunda mema kwa nchi za Afrika kutokana na wengi wao kupoteza msimamo baada
ya kutangazwa kwa mabilioni ya misaada ya mabadilko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea.
Ahadi za mabilioni hayo ya dola za kimarekani na
euro zilizotolewa na mataifa yaliyoendelea yameathiri kwa kiasi kikubwa
majadiliano ya mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa zimebadili
fikra na msimamo wa viongozi wa nchi zinazoendelea na kuacha kudai mambo muhimu
ya uwajibikaji kwa mataifa yanayoendelea kwa nchi za Afrika.
Katika andiko la tatu la mkataba wa mabadiliko ya
tabianchi ambalo limetoka Desemba 10, 2015 nchi za Afrika ziliondolewa kwenye
kundi la nchi zilizo kwenye mazingira magumu kwa kuathirika na mabadiliko ya
tabianchi jambo ambalo linatia doa msimamo wa awali wa Afrika.
Kuondolewa kwa Afrika kwenye kundi hilo kunamaanisha
kuwa Afrika itakosa misaada mingi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
hasa katika kutekeleza mchango wa kila nchi katika juhudi za dunia za
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Intended Nationally Determined
Contributions – INDCs).
Wachambuzi wa mambo wanasema ahadi hizo zimetumika
kama rushwa kushawishi wawakilishi wa Mataifa ya Afrika katika mkutano huo ili
wanyamaze na kuyakubali mapendekezo ya mataifa yaliyoendelea.
Katika majadiliano yaliyofanyika jana usiku, nchi za
Afrika hazikusema chochote ambapo wawakilishi wao waligeuka bubu na kutikisa vichwa
kuashirika kukubaliana na mapendekezo yaliyopo kwenye andiko la mkataba huo.
Wanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi wameendelea
kupaza sauti zao kupinga andiko hili wanalosema halikubaliki na kwamba limejaa
hadaa kubwa kwa nchi za Afrika.
“Afrika haijatambuliwa kwenye orodha ya mataifa zilizo
kwenye mazingira magumu kwa kuathirika na mabadiliko ya tabianchi tofauti na ilivyokuwa
kwenye andiko la awali, je kuna uwezekano wa jambo hili kubadilishwa kabla ya
kupitishwa kwa andiko?” anahoji Mithika Mwenda, Mratibu wa PACJA.
Mithika Mwenda, Mratibu wa PACJA |
Pamoja na nchi za kiafrika kunyamazishwa na ahadi
hizo za pesa zilipaswa kutambua kuwa hizo pesa ni ahadi ambayo hata hivyo
haijabainishwa wazi kwenye andiko la mkataba wa mazingira na kwamba kuna
asilimia nyingi kuwa ahadi hzio hazitatekelezwa.
Ahadi zilizowatia kiwewe mataifa ya afrika na hivyo
kuwaziba midomo kuchangia na kuweka shinikizo katika mambo ya msingi kwa bara
hilo ni pamoja na ahadi ya Austria ya EUR 500 milioni kati ya 2015 na 2020.
Ahadi nyingine ni kama ifuatavyo, nchi na kiwango
kwenye mabano Belgium (EUR 50 millioni), Canada (CAD 2.65 bilioni), Czech
Republic (USD 5.3 milioni), Denmark (USD 38 milioni), Estonia
(EUR 6 millioni), European Commission (EUR 2 billioni), Finland (EUR 500
Millioni), France (EUR 5 billion), Hungary (USD 4 million) wakati Germany ikiahidi
kuongeza msaada wake wa sasa maradufu kufikia 2020
Ahadi nyingine ni Iceland (USD 10 million), Ireland
(EUR 175 million), Italy (USD 4 billion ), Japan (Yen 1.3 trillion ), Lithuania
(EUR 100 000), Luxembourg (EUR 365 million ), Netherlands (EUR 440 million ),
New Zealand (NZD 200 million), Norway ( USD 400 million ), Poland (USD 8
million ), Spain ( EUR 900 million) na Uingereza (GBP 5.8 billion)
Majadiliano ya mkataba wa mabadiliko ya tabianchi bado
yanaendelea ambapo andiko la mwisho linatarajiwa kutoka jumamosi ya Disemba 12,
2015 na endapo wawakilishi wa mataifa ya Afrika wataendelea kulala ni dhahiri
mkataba huu utakuwa ni wenye kuyanufaisha mataifa yaliyoendelea.