Tanzania yahitaji zaidi ya USD 60 bilioni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Dotto Kahindi, Paris, Ufaransa Tanzania inahitaji kiasi cha dola za Kimarekani 65 bilioni sawa na bilioni 140 kwa mwaka kwaajili ya ... thumbnail 1 summary
Dotto Kahindi, Paris, Ufaransa

Tanzania inahitaji kiasi cha dola za Kimarekani 65 bilioni sawa na bilioni 140 kwa mwaka kwaajili ya kutekeleza mchango wake wa kila nchi katika juhudi za dunia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Intended Nationally Determined Contributions – INDCs).

Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Begum Karim Taj katika picha na Mwandishi wa blog ya Modewdj Andrew Chale
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP21, Jijini Paris, Ufaransa, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Begum Karim Taj ambaye pia alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli anasema kuwa mabadiliko ya tabianchi yameathiri rasilimali nyingi za taifa jambo linalohitaji fedha kukabiliana nayo.

Anasema mbali na athari za kuongezeka kwa kina cha bahari na kumeza baadhi ya visiwa, kuyeyuka kwa barafu wa Mlima Kilimanjaro, Ukame na Ukosefu wa maji vimechangia kushuka kwa pato la taifa kwa wastani wa asilimia moja kwa mwaka.

“Wakati wa kuandaa INDCs tumeona ni kwa namna gani mabadiliko ya tabianchi yamechangia katika kushuka kwa pato la taifa, ili kukabiliana na changamoto hii tunahitaji kiasi cha fedha kisichopungua usd 500 milioni” anasema Taj

Hata hivyo anasema kuwa pamoja na uwezo wake mdogo kifedha Tanzania imefanikiwa kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba wako tayari kufanya mengi zaidi endapo watapata msaada wa fedha, teknolojia na kujengewa uwezo.

Tanzania ikiwa na na hifahdi ya zaidi ya 53.28 trillioni cubic feet ya gesi,pamoja na nishati nyingine mbadala kama sola, upepo  imejikita katika kutumia nishati hiyo ambayo inachangia kwa kiasi kidogo uazalishaji wa hewa ukaa huku ikitoa uhakika wa nishati ya umeme kwa maendeleo ya uchumi wake.

Katika upande wa kuounguza makali ya mabadiliko ya tabianchi (Mitigation) Tanzania inahitaji kiasi cha dola bilioni 60 kwa mwaka hadi kufikia mwaka 2020.

Tanzania yenye hifadhi ya misitu ya ukubwa wa hekari milioni 48, sawa na ujazo wa 9.032 trilioni ya tone za kaboni, hivyo kuwa na hifadhi kubwa ya kaboni jambo ambalo inaamini ni mchango mkubwa katika kupunguza hewa ukaa.

“Ukiangalia INDCs yetu, utekelezaji wake unategemea sana namna ambavyo mataifa yaliyoendelea yatakavyotekeleza mahitaji kama tulivyoyanisha ambayo ni msaada wa fedha na teknolojia” anasema Taj

Anasema masuala ya maji, kilimo na mambo ya bahari ni vipaumbele vikuu kwenye INDCs na kwamba hawawezi kuyatekeleza kwa kutegemea nguvu yao pekee bila msaada wa mataifa yaliyoendelea.

Hivyo tunaomba mataifa yaliyoendelea kutekeleza ahadi zao kwa kusaidia utekelezaji wa INDCs kama makubaliano yalivyo kupitia Least Developed Country Fund, Adaptation Fund  na  Green Climate Fund

Taj anasema “Makubalino ya Paris yasiwe mzigo kwa nchi za Kiafrika ambazo bado zinajukumu kubwa la kupunguza uamsikini kwa wananchi wake, bali makubaliono yawe chachu ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea”