Uchambuzi : Mambo 7 yanayohitaji kurekebishwa kwenye andiko la kwanza la mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP21 Paris 2015

Dotto Kahindi, Paris, Ufaransa Desemba 9, 2015, Rais wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP21, Manuel Pulgar-Vidal... thumbnail 1 summary
Dotto Kahindi, Paris, Ufaransa

Desemba 9, 2015, Rais wa Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP21, Manuel Pulgar-Vidal ametoa andiko la kwanza la Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi baada ya majadiliano makali baina ya nchi zilizo wakilishwa kwa mkutano huo.

Mkataba huo unatarajiwa kupitishwa wiki hii baada ya kufikia makubaliano ambayo hata hivyo yanaonekana kuwa na ukakasi katika kuyafikia.

Baada ya kulipitia andiko la mkataba huu nimekuandalia mambo 7 ambayo yanahitaji kurekebishwa kabla ya kuingia makubaliano ya mwisho yatakayofanya andiko hilo kuwa shuruti kwa kila nchi mwanachama.

Utangulizi
Katika sehemu ya kwanza ya Mkataba huo inaanza kutumika lugha nguvu na inayojificha, jambo ambalo « linaweka upenyo wa nchi zilizoendelea kukwepa majukumu yao.

« Kwa mfano kwenye andiko kunakipengele kinachosema, nchi itasaidia kulingana na hali yake ya kiuchumi kwa wakati huo. Kipengele hicho kinapaswa kuondolewa »  anasema Fazal Issa Afisa Mirafi ForumCC

Nchi zinazoongoza kwa kuzalisha hewa ukaa kuwa na wajibu wa kusaidia nchi zinazoendelea kwa kuwa wa kwanza badala ya kuacha mzigo kwa nchi zinazoendelea.

Wastani wa joto
Asasi nchi nyingi zinataka wastani wa joto uwe 1.5 nyuzi joto, tofauti na inavyoonekana sasa kwa mataifa yalioendelea kutaka nyuzi joto 2. Kwenye andiko la sasa bado inaonyesha mambo yote mawili, ikiwa ni nyuzi joto 1.5 na nyuzi joto 2. Ni muhimu jambo hili kuamuliwa na kupata msimamo mmoja hasa ule unaoungwa mkono na watu wengi na wenye uhalisia ambao ni nyuzi joto moja na nusu.

Upunguzaji wa gesi Joto.
Fazal Issa anasema Tunataka kwamba mwaka wa kuanzia kupunguza gesi joto uanzia mwaka 1990 badala ya 2010 kama ilivyoandikwa katika andiko hili na kwa asilimia tunataka 75% katikati ya karne na 100% mwisho wa kanrne »

Kuna haja pi aya kuwepo kwa masharti ambayo yatahakikisha nchi zilizotoa ahadi zitekeleze ahadi na ili kufanikisha hilo nchi zilizoendelea zisisimamiwe bali zijisimamie zenyewe kufikia nyuzi joto hizo.

Kukabiliana na mabadiliko ya tabainchi
Juhudi zote zilenge katika kufikia kwenye nyuzi joto 1.5 na sio kama inavyoonekana hapa kwenye andiko hili la mkataba. Ikiwa ni pamoja na kiwango cha fedha ya misaada kiongezeke.

Inapaswa kuwa na uwazi mpana maana kwa andiko hili hakuna kilichoandikwa kwa tarakimu kuwa nchi zilizoendelea zitatoa kiasi gani cha fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Andiko hili limetambua umuhimu wa nchi zilizoendelea kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea.  Lakini hawatakiwi kuishia kutoa usaidizi tu bali kutambua kuwa ilo ni jukumu na wajibu wao.

Uharibifu na upotevu
Katika andiko hili bado hawajatambua kama jambo hili linaweza kuwa na ibara yake inayojitegemea lakini ni muhimu jambo hili liwe kwenye ibara yake inayojitegemea.

Kwa sababu toka Poland COP19 walikubaliana jambo hili ni muhimu, ni zaidi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na hivyo  ni vyema likasimama kwenye kipengele kingine badala ya kuliunganisha na mambo mengine.

Fedha za mabadiliko ya tabianchi.
Andiko hili limeficha mambo mengi kwenye mabano ambayo ndio hasa yanahitajika, haionyeshi ni kama fedha hizo zimeongezeka na kama zinatabilika zinakuja lini, kwa kiwango kinachotakiwa na kama  zinapatikana kwa njia rahisi.

Mfumo wa taasisi na kuanza kwa mkataba huo
Baada ya majadiliano ya Paris kumalizika, Katibu Mkuu wa COP atawaalika wanachama wote Aprili 22, 2016 ili kutia sahihi mkataba huu na utakuwa wazi kuridhia mpaka 2017.

Jambo ambalo haliko sawa hapa ni idadi ya wanachama wanaotakiwa kuasini ili kuupa nguvu ya kuanza kutumika mkabata huo ni 50 au 60 lakini kwa utaratibu wa kupata theluthi moja ya wanachama 196 namba inayokuja ni 65. Hivyo kuna haja ya andiko hilo kuonyesha idadi ya wajumbe 65 badala ya 50 au 60 inavyoonyesha sasa.

Jambo jingine ni lile la kunakujitoa kwa wanachama, ambapo mwanachama anaweza kuandika barua kwa katibu na kujitoa kwenye makubalinao na mkataba huo baada ya miaka mitatu, jambo hili linaweza kuondoa nguvu ya utekelezaji wa makubaliano hayo kwani nchi inaweza kujitoa kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Ni vyema kuwa na kipengele kitakachowezesha kufanyika kwa uchunguzi kubaini sababu za msingi zilizosababisha nchi husika kujitoa kwenye mkataba huo.

Ni hayo kwa sasa, tuendelee kusubiri andiko la mwisho la mkataba huu ambalo linatarajiwa kutoka kabla ya saa 24 kuanzia sasa.