Picha ni mnyama aina ya kasa ambaye anapatikana katika hifadhi ya taifa ya saadani iliopo mkoani Pwani
Na Woinde Shizza Pwani.
VIUMBE
wa baharini aina ya kasa wametajwa kuwa miongoni mwa viumbe wanaoishi
katika mazingira hatarishi huku wakitajwa kuwa wako hatarini kupotea
duniani kutokana na shughuli za binadamu na mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo
yamesemwa na mtaalamu wa kasa katika hifadhi ya taifa ya Saadan iliyopo
Bagamoyo mkoani Pwani,Hamis Abdallah wakati akizungumza na waandishi wa
habari waliotembelea katika hifadhi hiyo kujifunza vivutio mbalimbali
vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo.
Akiongea
na waandishi wa habari jana mtaalamu huyo alisema ya kwamba baadhi ya
wavuvi wamekuwa wakihatarisha maisha ya viumbe hao wanaopatikana
kandokando ya bahari ya Hindi inayopakana na hifadhi hiyo kutokana na
kuwavua hovyo .
Alisema
kwamba kasa huzaliana nchi kavu na ndiyo maana amekuwa akijijengea
baadhi ya maadui ambapo aliwataja kuwa ni papa,kenge ambao wamekuwa
wakishambulia mayai yao na kutishia uhai wa viumbe hao.
“Kasa
wanaishi katika mazingira magumu sana kwa kuwa wanaishi katika kina
kifupi cha maji na hivyo baadhi ya wavuvi huwavua hovyo lakini pia wana
tabia ya kuzaliana nchi kavu na sio majini”alisema mtaalamu huyo.
Hatahivyo,alisisistiza
ya kwamba kutokana na tishio la kutoweka kwa viumbe hao hifadhi ya
taifa ya Saadan imechukua hatua za haraka kuhakikisha wanachukua eneo
kubwa la bahari ili kuwahifadhi viumbe hao sanjari na kutunza mazingira
katika eneo hilo.
Alisema
kuwa hifadhi yao kupitia kitengo cha ujirani mwema kimekuwa
kikishirikiana na jamii inayoizunguka hifadhi hiyo kuhakikisha wanatoa
elimu ya kutosha kuhusu kutunza mazingira kwa lengo la kutoathiri
mabadiliko ya tabia nchi kwa maslahi ya viumbe hao.
“Tushirikiane
kutunza mazingira ili kuhifadhi hawa viumbe wa baharini kwa kuwa wana
faida kubwa sana kwa taifa endapo tutaendelea kuwatunza kasa
hawa”alisisitiza Abdallah
Hatahivyo,mtaalamu
huyo alifafanua kuhusu sheria za utunzaji wa viumbe wanaoishi baharini
na kusema kwamba sheria nambari 9 kifungu cha 12 inayohusu utunzaji wa
mazingira ya baharini ina sema iwapo mwananchi atahusika na uharibifu wa
viumbe walio hatarini kutoweka atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu
hadi mine.