Kufuatia
utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa kupanda miti kutunza Mazingira na
Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Raisi
Muungano na Mazingira, imetekeleza ahadi yake ya kugawa miche ya miti ya
matunda Mkoani Simiyu katika Majimbo ya ya Uchaguzi ya Busega, Bariadi,
Itilima, Kisesa, Meatu, Maswa Mashariki na Maswa Magharibi.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Raisi Mhe. Luhaga Mpina, amechangia miti ya
matunda ya maembe na machungwa ipatayo Elfu Kumi (10,000) huku,
Halmashauri na Wabunge wa Mkoa huo ,wamechangia idadi ya miche inayozidi
Elfu Kumi na Tatu (13,000).
Kwa
kuanzia idadi ya miche ya miti ya matunda ipatayo Elfu Kumi na Tatu Mia
Sita Sitini na Sita,(13,666) imeshapelekwa Mkoani simiyu ikiwa ni miti
ya maembe Elfu Kumi na Tatu na Mia Tano Sitini na Sita (13,566) na
Michungwa Mia Moja (100).
Awali,
Mhe. Mpina akitoa ahadi hiyo alisema, Mkoa wa Simiyu hauna miti ya
matunda ya kutosha hivyo Mkakati wa upandaji miti ya matunda utasaidia
chakula kwa familia, fedha kwa kuuza matunda na malighafi kwa viwanda
nchini na kusema kuwa miti ni Mali na miti ni uchumi.Aidha, Ofisi ya
Makamu wa Rais inamshukuru Mhe. Daudi Njalu Silanga (Mb). wa Itilima,
kwa kujitolea usafiri wa kusafirisha miche hiyo kutoka Chuo cha Kilimo
cha Sokoine kilichopo Mkoani Morogoro.
Idadi
ya miche elfu ishirini na saba (27,000) inatarajiwa kugawanywa katika
majimbo hayo, ikiwa ni pamoja na michango ya wabunge wa majimbo
hayo.Kupitia Mkakati huo wa Kitaifa wa kupanda miti na kuhifadhi vyanzo
vya Maji, Serikali pia imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika
kutunza mazingira na hususan wananchi wa Simiyu kuitunza miti hiyo ya
muda mfupi, ili kuiepusha nchi na hali ya jangwa na ukame.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA MAKAMU WA RAIS.