Wakulima, wanavyuo na wanaharakati wakutana kujadili bajeti ya serikali kwenye kilimo na mabadiliko ya tabiachi

Wanawake wakulima wadogowadogo wakiongozwa na waliokuwa washiriki wa Shindano la Mama Shujaa wa Chakula linaloratibiwa na shirika la Oxf... thumbnail 1 summary
Wanawake wakulima wadogowadogo wakiongozwa na waliokuwa washiriki wa Shindano la Mama Shujaa wa Chakula linaloratibiwa na shirika la Oxfam, wamekutana pamoja na wadau kutoka taasisi mbalimbali na baadhi ya wanafunzi kutoka elimu ya juu, Tanzania kujadili Bajeti ya Kilimo kwa mwaka 2016/17 na changamoto za mabadiliko ya Tabianchi.

Meneja utetezi wa Oxfam Tanzania, Eluka Kibona anasema Mkutano huo wa siku tatu umewakutanisha wadau hao ili kuijadili Bajeti ya serikali katika sekta ya Kilimo na Mabadiliko ya Tabianchi.

Imekuwa ni kawaida kwa bajeti ya kilimo kuletwa mezani bila wakulima wengi hasa wadogowadogo kushirikishwa katika masuala ya bajeti hiyo, hivyo mkutano huo utasaidia kuibua changamoto mbalimbali na namna ya utatuzi wake katika sekta ya kilimona mabadiliko ya tabianchi.
 

Meneja Mradi, Forum CC, Rebecca Muna anasema mabadiliko ya Tabianchi yanaathiri zaidi wakulima wadogowadogo hasa waliopo vijijini, hivyo kupitia mkutano huo wakulima wanapata elimu ili kukabiliana na mabadiliko hayo.

Akieleza kwa undani juu ya Mabadiliko ya tabia nchi mwezeshaji kutoka Forum CC, Fazal Issa alisema kwamba changamoto kubwa zaidi ya mabadiliko ya Tabia nchi ni pamoja na maji chumvi kuingia nchi kavu na kuathiri ukuaji wa mazao, kuongezeka kwa joto, misimu ya mvua zisizotabirika, kupungua kwa kina cha maji katika mito na maziwa, kuongezeka kwa majanga ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na mafuriko, ukame na vimbunga na kuongezeka kwa magonjwa ya mazao.

Alisema kuwa mambo yote hayo yamekuwa yakichochea wakulima na wafugaji kukosa maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo, hivyo ili wakulima waweze kukabiliana na changamoto hiyo ya mabadiliko ya Tabia nchi wanatakiwa kujifunza mbinu mbalimbali ikiwemo kuvuna maji ya mvua, kutumia umwagiliaji wa matone, matumizi ya mbegu bora zinazostahimili magonjwa na Ukame, kilimo mchanganyiko/mseto, matumizi ya mbolea asili na kuongeza thamani ya mazao.

Nao wakulima hao kwa nyakati tofautitofauti walizungumzia suala zima la bajeti ambapo walisema kuwa changamoto nyingi wanazozipata kwa kutoshirikishwa kwenye bajeti kuu juu ya kilimo zinasababisha wasifikiwe na elimu na huduma mbalimbali zitakazowasaidia kwenye shughuli zao za kilimo.


Hata hivyo, wameiomba serikali kusikiliza maoni yao hasa wakati wa uandaaji wa bajeti kwa ujumla kwa kuwa wao ndiyo walengwa namba moja kwenye sekta ya kilimo nchini.

Meneja utetezi kutoka Shirika la Kimataifa la OXFAM Tanzania Bi. Eluka Kibona akifungua mafunzo juu ya uelewa wa Bajeti ya Kilimo na Mabadiliko ya Tabianchi yanavyoathiri sekta ya kilimo Tanzania hasa wakulima wadogo wadogo.
Meneja Mradi, Forum CC, Rebecca Muna akielezea umuhimu wa mafunzo hayo yatakavyoweza kuwasaidia wakulima wadodogo katika kukabiliana na tatizo la Mabadiliko ya tabianchi.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo wakiwa katika kikundi kujadiliana maswala mbalimbali juu ya namna ya kuandaa bajeti.
Baadhi ya wadau waliohudhuria mafunzo hayo wakiwa wanatazama mfano wa jarida linalo onesha jinsi bajeti inavyo andaliwa.

Washiriki wakifuatilia mafunzo hayo.
 


Chanzo: Habari-Blog za mikoa, Picha-Fredy Njeje, Uhariri-Tabianchi