Wakuu wa Wilaya za Arusha kusimamia Mradi wa Mabadiliko ya Hali ya hewa Na Tabia ya Nchi

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Mrisho Gambo(Kushoto) akibadilishana business card Mwakilishi Mshauri wa Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na ... thumbnail 1 summary
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Mrisho Gambo(Kushoto) akibadilishana business card Mwakilishi Mshauri wa Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) Alais Morindat.

Mwakilishi Mshauri wa Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) Alais Morindat (aliyesimama)akiwasilisha mada ya kutambulisha mradi wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabia ya Nchi kwa Sekretariet ya Mkoa wa Arusha
Viongozi wa Mkoa wakifuatilia mawasilisho ya mradi wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabia ya Nchi ambao unatekelezwa kwa awamu ya pili katika Wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro
Mratibu wa Mradi kutoka Tamisemi Sanford Kway akielezea wajibu wa Wizara katika kusimamia Mradi huu wa Mabadiliko ya hali ya hewa na tabia ya nchi katika halmashauri 15 Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo akitoa maelekezo katika kikao cha kutambulisha Mradi wa Mabadiliko ya hali ya hewa na Tabia ya Nchi.


Teghenjwa Hoseah, Arusha .

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe Mrisho Gambo amewaagiza Wakuu wa Wilaya tatu za Mkoa wa Arusha zinazotekeleza mradi wa mabadiliko ya hali ya hewa na tabia ya nchi kuwa Wenyeviti wa kamati za mradi huo ili kuharakisha utekelezaji wake katika maeneo hayo. 

Akizungumza katika kikao cha kutambulisha mradi huo wa awamu ya Pili utakaofanya kazi katika wilaya za Ngorongoro, Monduli na Longido za Mkoa wa Arusha kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016 hadi 2021 alisema kuna haja ya kuimarisha usimamizi wa mradi huu ili kuwajengea uwezo wanajamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ili mradi huu uweze kuleta Tija iliyokusudiwa. 

Alisema awali kamati hizo zilikuwa zikisimamiwa na Maafisa Mipango katika halmashauri hizo ila kutokana na majukumu yao ameonyesha wasiwasi iwapo wanaweza kuusimamia ipasavyo hivyo aliwataka Wakuu wa wilaya kuwa vinara wa kuusimamia na kuratibu kwa karibu ili kuleta mapinduzi katika maeneo ya wafugaji na kuhakikisha wanatengeneza mfumo imara na utekelezaji wa mradi huo unafanikiwa kuanzia ngazi ya kijiji. 

“Nahitaji kuona halmashauri ambazo zinatekeleza mradi huu ifikapo mwezi Novemba ziwe zimeshaanza kutekeleza majukumu yake bila vikwazo vyovyote na nipate taarifa zake mara kwa mara ili fedha zilizotolewa na wafadhili zilete matokeo chanya,”alisema Gambo 

Akizungumza wakati wa Kikao hicho Mwakilishi Mshauri wa Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo (IIED) Alais Morindat alisema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa imekua ni tishio kubwa kwa wananchi haswa wa maeneo haya ya wafugaji na ndio maana tulianza na Halmashauri hizi kutokana na athari zilizojitokeza katika jamii za wafugaji ambapo mifugo mingi katika maeneo yao ilipoteza uhai. 

Aliongeza kuwa mradi huu unatofauti na miradi mingine tuliyoizoea kwa sababu Jamii inakuwa na nafasi ya kuamua jinsi Fedha za Mradi zitakavyotumika huku malengo ya mradi yakiwa ni kuijengea uwezo Ofisi ya Raisi –TAMISEMI katika maeneo makubwa mawili ambayo ni uimarishaji wa taasisi katika uratibu wa mradi na uwezo wa kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kuziwezesha mamlaka za serikali za mitaa hapa nchini ziweze kutoa elimu kwa jamii kutambua na kutekeleza Miradi ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi 

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo hususan Shirika la Kimataifa la Mazingira na Maendeleo (IIED), Haki Kazi Catalyst (HKC), Jumuiko la Maliasili Tanzania(TNRF) chini ya ufadhili wa Serikali ya Uingereza (UK-aid) na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNCDF LoCAL) itatekeleza mradi huu katika Halmashauri 15 huku zaidi ya Bilioni 6 zinatarajia kutumika katika mradi huu.