Serikali yatoa onyo kali kwa waliovamia hifadhi za misitu Geita

Na Hamza Temba - WMU Wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu na wanyamapori nchini wametakiwa kutii sheria za uhifadhi na kujiepush... thumbnail 1 summary
Na Hamza Temba - WMU

Wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu na wanyamapori nchini wametakiwa kutii sheria za uhifadhi na kujiepusha na vitendo viovu vya uharibifu wa mazingira vinavyopelekea kupotea kwa uoto wa asili na kutishia nchi kuwa jangwa ambapo pamoja na mambo mengine wametakiwa kuondoa mifugo yao katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria. 

Hayo yamesemwa juzi Mkoani Geita na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa huo Wilayani Chato kuhusu maelekezo ya kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo hifadhi Mkoani humo na taifa kwa ujumla.

Alieleza kuwa vitendo hivyo vya uharibifu wa mazingira ni pamoja na ukataji wa miti hovyo, kilimo kisichoendelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji makazi na shughuli zingine za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwemo Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Taifa.

"kwa sasa Tanzania inapoteza takriban hekta 372,000 za uoto wa asili kila mwaka na endapo hali hiyo ikiachwa iendelee tishio la kutoweka kwa uoto huo ni kubwa zaidi. Takwimu pia zinaonyesha kuwa Tanzania ina eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa takriban Hekta milioni 48.1 na kwamba kasi hiyo ikiachwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129" alisema Makani.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi wa eneo la Mchangani waliovamia Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo – Kahama uliopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita alipotembelea kuona changamoto za uhifadhi. Asilimia 70 ya hifadhi hiyo kwa upande wa Wilaya ya Chato imeharibiwa kabisa na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ufugaji na makazi ya kudumu, nyumba zinazoonekana pichani na sehemu ya makazi hayo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani akionesha moja ya kigingi (beacon) cha mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa Biharamulo - Kahama uliopo Wilayani Chato Mkoa wa Geita ambao umevunjwa na wananchi waliovamia msitu huo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Gen. Mstaafu Ezekiel Kyunga na Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe (kulia).
Hizi ni miongoni mwa athari za uvamizi wa wananchi hao katika Hifadhi ya Misitu wa Biharamulo - Kahama Wilayani Chato Mkoa wa Geita ambapo miti ya asili imekatwa kupisha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi bila kujali athari za tabianchi. 

Chanzo: Michuziblog