Wajasiriamali wa GO BIG kuanzisha kijiji cha maendeleo

Na Naamala Samson Wajasiriamali waundao mtandao wa maendeleo wa GO BIG yaani “GO BIG DEVELOPMENT NETWORK” wanatarajia kukusanya zaid... thumbnail 1 summary
Na Naamala Samson

Wajasiriamali waundao mtandao wa maendeleo wa GO BIG yaani “GO BIG DEVELOPMENT NETWORK” wanatarajia kukusanya zaidi ya kiasi cha shilingi milioni mia mbili na hamsini (250) ili kuanzisha kijiji cha mfano. Kijiji hicho kinatarajiwa kuanzishwa mwishoni mwa mwaka huu na kitahusisha shughuli mbalimbali za wajasiriamali hao.

Akichangia katika sherehe za kutimiza mwaka mmoja wa umoja huo zilizofanyika Vikindu nje kidogo ya jiji la Dar Es Salaam mnamo mwanzoni mwa mwaka huu, mmoja wa walezi, Bwana Andrew Mhina aliwaambia wajasiriamali hao, “ndugu zangu, wakati ni huu ambapo tukianzisha kijiji cha mfano cha ‘GO BIG VILLAGE’, watu tutaweza kulima humo, kufuga, kuzalisha bidhaa kwa wingi na kwa ubora kukidhi sio tu soko la ndani bali na la nje”. Aliongezea kwa kusema kuwa watatumia kijiji hicho kuongeza ajira na kujenga taifa la watu kuwa wabunifu zaidi.
 Mgeni rasmi, Bw.David kutoka shirika la nyumba la taifa (NHC) kama Mkurugenzi wa kitengo cha uwekezaji akiwahamasisha wajasiriamali wa GO BIG. Kulia ni mlezi wa wajasiriamali hao, Bw.Andrew Mhina na Kushoto ni Bi.Nancy Msangi, makamu mwenyekiti wa umoja huo (Picha na Naamala Samson)
 Waanzilishi wa umoja wa GO BIG, Bwana Meshack Maganga akiwa na Bwana Mwimba Philemon ambaye pia ni mweka hazina wa umoja huo (Picha na Naamala Samson)

“Ni lazima tuwe vijana wa mfano, tuwe wajasiriamali wa mfano sio kwa maneno bali kwa vitendo na tuweke nia sasa ya kuanzisha kijiji hiki kitakachotusaidia sisi na kuinua uchumi wa nchi yetu.”, alisema Bwana Meshack Maganga ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa umoja huo wa wajasiriamali wa GO BIG.

Umoja huo unaundwa na watu mbalimbali takribani mia mbili na hamsini wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji na utoaji huduma na wanatarajia kuchangishana kila mmoja milioni moja kwa kuanzia. Na kuzitumia milioni mia mbili na hamsini (250) kama kianzio kununua eneo kubwa katika mkoa utakaoteuliwa na kisha kuendelea kuanzisha katika mikoa mingine.

Akiwapa moyo wajasiriamali wengine hasa wanawake, Bi.Sarah Filikunjombe alisema, “dada zangu na wadogo zangu hasa wa kike, msivunjike moyo mnapoona mnapoona mnapata changamoto kwenye kulima. Mimi nimeshapata sana hasara kwenye kilimo cha vitunguu, matikiti na hata kwenye kufuga kuku lakini sikati tamaa na ninasonga mbele.”

Wajasiriamali hao walitoa rai kwa serikali kuhakikisha inasaidia wajasiriamali wa ndani ili kuwainua kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuendeleza ubunifu wao, kuwatengea maeneo maalum ya kufanyia shughuli zao bila bugudha, na kuwalegezea masharti ya kupatikana kwa mkopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha.

Pamoja na hayo, wajasiriamali hao wa GO BIG wanaotoka sehemu mbalimbali nchini, waliweza kubadilishana uzoefu na kuhamasishana katika kilimo cha miti ya mbao, ufugaji nyuki, kilimo cha vitunguu, matikiti, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na shughuli kadhaa za huduma za chakula, huduma za kiteknolojia, vinywaji na utoaji wa mafunzo mbalimbali, na nyinginezo nyingi.
 Wajasiriamali wakifuatilia mazungumzo
Sarah Filikunjombe akiongea na wajasiriamali wenzake wa GO BIG