MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA WADAU WA MAZINGIRA JIJINI DAR ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao cha Wadau wa Mazingira kuhusu Changamoto ya... thumbnail 1 summary

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao cha Wadau wa Mazingira kuhusu Changamoto ya Mafuriko na Hifadhi ya Mazingira katika mkoa wa Dar es Salaam (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameongoza kikao cha Wadau wa Mazingira kuhusu Changamoto ya Mafuriko na Hifadhi ya Mazingira katika mkoa wa Dar es Salaam, kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo kwenye ofisi ya Makamu wa Rais mtaa wa Luthuli.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na mafuriko katika jiji la Dar es Salaam.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa mkutano na Wadau wa Mazingira kuhusu changamoto ya mafuriko na hifadhi ya mazingira katika mkoa wa Dar es Salaam.

Makamu wa Rais alisema kulikosekana umakini katika kusimamia mazingira na miundo mbinu katika jiji la Dar es Salaam.

Makamu wa Rais alizungumzia changamoto za kuwepo kwa taka ngumu ambazo zingeweza kuzalisha umeme na gesi, “kuna miradi watu wanaomba kuzalisha umeme kwa taka, anazungushwa mtu miaka mitano, sita , saba, haambiwi ndio wala haambiwi hapana “

Makamu wa Rais amesema kuna uhitaji sana wa elimu ya mazingira kwa jamii na kupeana taarifa mbali mbali zinazohusiana na mazingira .

Makamu wa Rais alisema moja ya tatizo kubwa ni kuchukua nyezo za uthibiti kufanya nyenzo za mapato “Vibali, leseni hivi ni vitu vinavyotolewa kwa ajili ya uthibiti lakini tumevigeuza kuwa vyombo vya mapato” kutokana na hali hiyo vibali vimeendelea kutolewa hovyo bila kuzingatia taratibu.

Makamu wa Rais alitoa maagizo ya kuundwa kwa Kamati ya Mazingira ya mkoa wa Dar es Salaam ambayo itaundwa na  Waziri wa Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba na kuratibiwa  na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda.

Makamu wa Rais aliwashukuru wadau wa maendeleo wakiongozwa na Benki ya Dunia katika kusaidia kupambana na tatizo la uharibifu wa mazingira na mafuriko jijini Dar es Salaam.

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba alisema ni wakati wa kutafakari na kupata jawabu la kudumu la suala la mafuriko yanayotokea katika jiji la Dar es Salaam.