WADAU WAKUTANA KUJADILI MABADILIKO YA TABIANCHI

 Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Fadhila Khatib akifungua... thumbnail 1 summary
 Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Fadhila Khatib akifungua warsha ya wadau kuhusu usimamizi jumuishi wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi maeneo ya Pwani, warsha hiyo inaendelea katika Ukumbi wa NIMR Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki wa warsha jumuishi ya usimamizi wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi maeneo ya Pwani wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi (hayupo pichani).
 Washiriki wa warsha jumuishi ya usimamizi wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi maeneo ya Pwani wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Bi. Fadhila Khatib.

Imeelezwa kuwa mabadiliko ya Tabianchi yanasababisha athari mbalimbali kama vile ukame, mafuriko, kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, kumezwa kwa visiwa na kuongezeka kwa ujazo wa maji ya bahari unaosababishwa na kuyeyuka kwa barafu katika ncha za Dunia. 
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Dkt. Fadhila Khatib wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau kuhusu usimamizi jumuishi wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi maeneo ya Pwani.
Mhandisi Malongo amesema kuwa hasara za athari hizo ni kubwa zaidi katika bara la Afrika kwa kuwa uchumi wake ni tegemezi kwa hali ya hewa na pia uwezo mdogo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na umaskini.
Hata hivyo ripoti ya wataalamu iliyotolewa mwaka 2011 kuhusu gharama za kiuchumi zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi zinaweza kufikia asilimia mbili 2% ya Pato la Taifa kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.
“Wadau wa mwambao wa Pwani katika mtandao wenu mliouanzisha chini ya mradi huu mnao wajibu wa kuweka kipaumbele kwenye kutafuta mikakati ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi” Malongo alisisitiza.
Kwa upande mwingine Msimamizi wa Mradi huo Dkt. Kanizius Manyika amesema kuwa mradi umekamilika kwa asilimia 99 na umefanikiwa kuvuka malengo yaliyokusudiwa kwa kutoa majiko banifu zaidi ya 3000 katika Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, Ujenzi wa mtaro Ilala Bungoni wenye urefu wa Mita 475 na Mtoni-Mtongani Mita 550. Pia ujenzi wa ukuta wa wenye urefu wa mita 920 barabara ya Barack Obama na Mita 380 katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni.
Mradi huo ambao shughuli zake zimekamilika umechangia kutatua baadhi ya changamoto zinazosababibishwa na kuongezeka kwa usawa wa maji ya bahari ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma juu ya mabadiliko ya tabiachi na athari zake na upandaji wa Mikoko katika jiji la Dar es Salaam.