Na Mwandishi wetu
Katika
jitihada za kutunza mazingira na kupunguza kasi ya ukataji miti ili kupata
nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) linasambaza gesi asilia kwa
ajili ya kupikia majumbani badala ya kutegemea kuni na mkaa.
Mradi
huo wa TPDC unaolenga kufikisha nishati hiyo majumbani ulianzia Mikocheni, Dar
es Salaam na sasa unaelekea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ukitarajiwa
kuwapatia huduma hiyo wakazi wanaoishi kwenye mitaa iliyopimwa kwanza.
Dar
es Salaam yenye wakazi zaidi ya milioni tano watu milioni 4.9 hupikia nishati
ngumu ikiwemo kuni na mkaa wakati wachache hutumia gesi, umeme na mafuta ya
taa.
Mhandisi
wa Petroli wa TPDC, anayeshughulia mradi huo, Modestus Lumato, aliliambia
NIPASHE Jumapili, katika mahojiano ya jitihada za TPDC katika kutunza mazingira
na kuendeleza matumizi ya nishati mbadala majumbuni.
Alifahamisha
kuwa mradi huo unasambaza gesi asilia inayotoka Songosongo mkoani Lindi lakini
pia utatumia ile ya Mtwara baada ya ujenzi wa bomba jipya la gesi la Mtwara
–Dar kukalimika mwakani. Alisema ufungaji ulianzia kwenye nyumba za TPDC
Mikocheni ambazo wakazi wake wameanza kuitumia.
Aliongeza
kuwa sehemu zenye ramani za mitaa zote zitafikiwa na usambazaji huo unaohusisha
kujenga bomba la gesi na kuwafikishia watumia watakaonunua kwa mtindo wa
“LUKU’.
“Tutaanza
muda wowote kusambaza nje ya TPDC baada ya pesa kupatikana toka Hazina. Ni
mradi unaosimamiwa na TPDC na ni mali ya serikali kwa asilimia mia. Bajeti ya
Sh bilioni 30 imetengwa kwa ajili ya kusambaza mabomba ya gesi Dar es Salaam.”
Lumato
alifahamisha kuwa kazi ya kusambaza gesi asili ikikamilika jijini TPDC
itaendelea mikoani kama Mtwara na Lindi ambapo nishati hiyo inapatikana kwa
wingi.
Akitofautisha
gesi asili na ile inayotumika majumbani sasa , Lumato alisema ile ya asili ni
nishati rahisi mno duniani ikilinganishwa na ya viwandani iitwayo ‘Liquid
Petroleum Gas’ (LPG) inayotokana na kusafisha mafuta ghafi , lakini ile ya
asili inatokana na kuoza masalia ya viumbe hao waliokufa miaka milioni kadhaa
iliyopita.
Aliongeza
gesi asili ni nafuu kwani mteja aliyekuwa anatumia mitungi miwili ya LPG ya
kilo 15 kwa mwezi atapunguza gharama kwa kutumia gesi asili ya Sh. 50,000 kwa
miezi sita. Mtungi wa kilo 15 wa LPG huuzwa Sh. 55,000.
Tanzania
imegundua tabaka la gesi lenye ujazo wa fiti za mraba trilioni 35 zilizopatika
mikoani Mtwara na Lindi na ujenzi wa bomba la kuisafirisha kutoka Mtwara kuja
Dar es Salaam unaofanywa na mkandarasi kutoka China umeanza na utarajiwa
kukamilika baada ya miezi 18.
Kadhalika
iligundua fiti za mraba trilioni tatu eneo la Mnazi Bay na kiasi kingine cha
fiti trilioni mbili zipo katika kisiwa cha Songo Songo ambazo hutumika
kuzalisha umeme na kwenye baadhi ya viwanda.
Chanzo: Nipashe
Jumapili