Baa la njaa latishia wakazi 6790

Tabora. VIJIJI vitatu katika Kata ya Ndevelwa, Manispaa ya Tabora viko hatarini kukumbwa na njaa, hali ambayo imetishia wakazi zaidi ya... thumbnail 1 summary
Tabora.
VIJIJI vitatu katika Kata ya Ndevelwa, Manispaa ya Tabora viko hatarini kukumbwa na njaa, hali ambayo imetishia wakazi zaidi ya 6790 waishio kwenye vijiji hivyo.
Wakazi wa vijiji vya kata ya Ndevelwa tayari imebainika kuwa wamekuwa wakila mlo mmoja kwa siku na wengine hata kupitisha siku nzima bila kula.
Akizungumza na gazeti hili,Diwani wa kata ya Ndevelwa Seleman Maganga, amekiri kuwepo kwa hali hiyo huku akiitaka serikali kuchukua juhudi za makusudi kukabiliana na janga hilo.
Maganga alisema tatizo hilo ni matokeo ya hali ya ukame iliyovikumba vijiji hivyo tangu mwishoni mwa mwaka jana,na tayari amekwishalifikisha kwenye vikao vya baraza la madiwani na kujadiliwa.
Alifafanua kuwa kwa upande mwingine hali hiyo imechangiwa na idadi kubwa ya vijana waishio vijiji vya Inala,Ituru na Ndevelwa kutoshiriki shughuli za kilimo hata cha bustani  na kuwaachia wazee peke yao ambao huzalisha kidogo kulingana na uwezo wao.  
Aidha alisema idadi kubwa ya vijana wamekuwa wakikimbilia mjini na wale wanaobaki vijijini hujihusisha na vitendo vya kihalifu ili mradi kujihakikishia kipato kisicho cha halali.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa vjijiji hivyo waliolima zao la muhogo wanalazimika kuuza madebe mawili kwa Sh16,000 ili wakanunue debe moja la mahindi, ambalo wanadai kuwa ndio linatosheleza kwa mlo wa siku saba katika familia moja.
Mwaka 2010  serikali ilitoa chakula cha msaada baada ya vijiji hivyo vya kata ya Ndevelwa kukumbwa na mvua kubwa iliyoharibu mazao ya chakula na biashara kama tumbaku na mahindi.

Chanzo: Mwananchi