HALI YA BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU BADO TETE, UVUVI HARAMU WAKITHIRI

Na Florah Temba, Moshi-Kilimanjaro Yetu LICHA ya serikali mkoani Kilimanjaro kulifunga bwawa la Nyumba ya mungu kwa kipindi cha miezi... thumbnail 1 summary
Na Florah Temba, Moshi-Kilimanjaro Yetu

LICHA ya serikali mkoani Kilimanjaro kulifunga bwawa la Nyumba ya mungu kwa kipindi cha miezi sita kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa uzalishaji wa samaki, hali katika bwawa hilo bado imeelezewa kuwa mbaya kutokana na kuendelea kuwepo kwa vitendo vya uvuvi haramu  vinavyoendeshwa kwa wizi.

Bwawa hilo lililoko wilayani Mwanga Mkoani Kilimajnjaro, lilifungwa Mwezi Februari mwaka huu, kwa ushirikiano wa serikali ya mkoa wa Kilimanjaro na Manyara, kutokana na kupungua kwa kina cha maji na kushamiri kwa uvuvi haramu.

Wakati Bwawa hilo linafungwa samaki walikuwa wamepungua kutoka Tani zaidi ya 5,000 zilizokuwa zikizalishwa kwa mwaka, hadi kufikia Tani 1770 kwa mwaka hali ambayo ilionekana kuathiri sekta ya uvuvi.

Bwawa hilo ambalo lilitakiwa kufunguliwa Septemba Mosi mwaka huu, bado halijafunguliwa na linaelezewa kufunguliwa wakati wowote kuanzia sasa ingawa bado haijafahamika kama samaki wameongezeka au la.

Akizungumza   mkuu wa wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro Bw. Shaibu Ndemanga, alikiri kuendelea kushamiri kwa vitendo vya uvuvi haramu katika Bwawa hilo, licha ya kwamba bado halijafunguliwa.

Alisema pamoja na Bwawa hilo kufungwa kwa nia njema ya kuacha samaki wawe wakubwa, bado vitendo vya uvuvi haramu vilikuwa vikiendelea kwa wizi hali ambayo inaonekana kurudisha nyuma jitihada za mkoa huo za kuinua sekta ya Uvuvi.

“Ni kweli bwawa hili lilifungwa kwa miezi sita na lilitakiwa kufunguliwa tarehe moja mwezi wa tisa, lakini bado halijafunguliwa na tutalifungua wakati  wowote kuanzia sasa ,kwani yapo mambo  ya Msingi  ambayo yanapaswa kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya namna ya kulinda  samaki”alisema

Hata hivyo mkuu huyo alipoulizwa kama samaki wameongezeka alisema bado takwimu hazijatolewa na kusisitiza kuwa pamoja na kufungwa kwa bwawa hilo  wizi wa samaki ulikuwa ukiendelea kwa kiasi kikubwa.

Akizungumzia suala la ulinzi Bw. Ndemanga alisema ulinzi katika bwawa hilo unahitaji rasilimali nyingi ikiwemo Mafuta kutokana na kwamba wavuvi huingia usiku kwa kificho na kuendeleza uvuvi haramu jambo ambalo ni hatari kwa uzalishaji wa samaki.

 Alisema wakati bwawa hilo linafungwa yapo mambo mbalimbali ambayo yalitakiwa kutekelezwa kabla halijafunguliwa ikiwa ni pamoja na vyombo vya uvuvi kusajiliwa,watu kujisajili,kuundwa kwa vikundi na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Bwawa  kuanzisha miradi mingine ya maendeleo ili kuondokana na hali ya kutegemea bwawa hilo kama njia pekee ya kuwaingizia kipato.

Bwawa hilo linatumiwa na wilaya Tatu ikiwemo wilaya ya Mwanga ambayo inawavuvi zaidi ya 3.000 na ambao wameshajisajili hadi sasa ni wavuvi 600 pekee.

Chanzo: Kilimanjaro Yetu