HUDUMA YA MAJI KUWAFIKIA WAKAZI 9,000

Na Mwandishi wetu, Handeni MKUU wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano wakati wa u... thumbnail 1 summary
Na Mwandishi wetu, Handeni
MKUU wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi wa uchimbaji visima virefu 15 vitakavyosaidia huduma ya maji kuwafikia wakazi 9,000.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa hivi karibuni, wakati wa makabidhiano ya hundi ya zaidi ya Sh milioni 40, iliyotolewa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa mkandarasi anayechimba visima hivyo ambaye ni Kisangani Smith Group wa mkoani Njombe.


Alisema huduma hiyo itawafikia wakazi wa Vijiji vya Ngojoro, Kwamgwe, Kwadoya na Bondo, vinavyounda Kata ya Kwamgwe.

“Maji yanapungua kwa kasi katika maeneo mbalimbali duniani kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa na binadamu, tambueni kwamba TBL wamefadhili ujenzi, lakini jukumu la kutunza visima ili viwe chanzo endelevu ni la kwetu sisi.

“Kwamgwe mnayo bahati kuchaguliwa kupata maji, hasa tukizingatia kwamba wananchi wengi wa Handeni hawana maji na wanahangaika, kwa hiyo litakuwa jambo la aibu kama itapita miezi michache tukakuta miundombinu ya visima imeharibika au havitoi maji kabisa,” alisema Rweyemamu.

Alisema kukamilika kwa visima hivyo kutaleta ukombozi kwa wanakijiji wa kata hiyo, hasa wanawake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uhusiano na Sheria wa TBL, Stephen Kilindo, alisema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya mikakati ya kampuni hiyo kuchangia juhudi za maendeleo katika jamii.

“Kazi ya kuchimba itakamilika ndani ya miezi mitatu ijayo, shughuli hii ni utekelezaji wa kampeni yetu ya hakuna maji hakuna uhai tunayoiendeleza katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo kwa mwaka huu shilingi milioni 300 zimetumika,” alisema Kilindo.
Chanzo: Mtanzania