JK: TUVUTE SUBIRA MGOGORO ZIWA NYASA

Na Mwandishi Wetu RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kuwa na subira kuhusu tatizo la mpaka wa Ziwa Nyasa. Alisema katika kushughu... thumbnail 1 summary
Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kuwa na subira kuhusu tatizo la mpaka wa Ziwa Nyasa.

Alisema katika kushughulikia utata wa mpaka huo na nchi ya Malawi, Tume maalumu ilikuwa ikutane Septemba 10 hadi 15 mwaka huu lakini mkutano huo haukufanyika.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana katika hotuba yake ya kila mwezi kwa Watanzania na kusisitiza kuwa, nchi ya Malawi iliomba mkutano huo usogezwe mbele.

“Sisi tumekubali ombi lao hivyo tunawasubili kwani subira yavuta heri, upande wetu tunaendelea na matayarisho husika kama tutaamua kwenda Mahakama ya Kimataifa (ICJ) nchini Uholanzi,” alisema.

Alitoa wito kwa Watanzania kuitunza na kudumisha amani iliyopo kwa kuheshimu misingi ya katiba, kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria, kuheshimiana na kuvumiliana kwa tofauti zetu.

“Wananchi wenzangu tuione tunu hii ya amani tuliyonayo kuwa ni ya kuitunza kama mboni ya macho yetu badala ya kuibomoa, wako wenzetu wanaitafuta hawaipati.

“Amani ikitupotea si rahisi kuipata na hata ikirudi madhara yake mtaishi nayo miaka mingi au hata kudumu daima, ni rahisi sana kubomoa nyumba iliyojengwa kwa siku nyingi kwa uzembe wa siku moja tu, lakini kuijenga upya itachukua muda,” alisema Rais Kikwete.

Mkutano wa AGRA

Akizungumzia Mkutano Mkuu wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), Rais Kikwete alisema umeiletea sifa na heshima kubwa Tanzania.

Alisema kati ya asilimia 70-80 ya watu katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea kilimo ambacho ndio chanzo kikuu cha ajira kwa watu waishio vijijini. 

Aliongeza kuwa, kilimo hutoa mchango mkubwa kwenye pato la Taifa la nchi nyingi pia ndio chanzo kikubwa cha fedha za kigeni na malighafi za viwandani ambapo kutokana na umuhimu wake kama hakijastawi vizuri barani Afrika, hali za watu wengi zinakuwa duni, uchumi wa nchi kudorora na maendeleo kudumaa.

“Katika mkutano huu tulikubaliana kwa pamoja kuwa bila kuongeza uwekezaji na matumizi ya maarifa mapya katika kilimo chetu, uzalishaji hautaongezeka Afrika.

“Tatizo la upungufu wa chakula na njaa litaendelea na watu wengi hasa wa vijijini watabakia kuwa maskini, hivi sasa watu wapatao milioni 239 barani Afrika wanaishi bila ya uhakika wa chakula.

“Hiki kimekuwa chanzo kimojawapo cha utapiamlo na vifo vya akina mama wajawazito na watoto katika nchi za Afrika,” alisema.



Miaka 20  ya vyama vingi

Alisema katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, tumeona maendeleo makubwa ya ukomavu wa demokrasia inavyozidi kushamiri.

Wananchi wa Tanzania wamepata uhuru wa kuanzisha na kujiunga na vyama vya siasa, uhuru mkubwa zaidi wa kufanya na kushiriki katika shughuli za kisiasa, kufanya maandamano na kuitisha mikutano ya hadhara ya kisiasa, kijamii na mingineyo.

Aliongeza kuwa, hivi sasa wananchi wana uhuru mkubwa wa kutoa maoni yao kupitia majukwaa ya mikutano ya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya habari au mitandao ya intaneti na simu za mikononi. 

Utendaji wa vyama vya Siasa

Rais Kikwete alisema CCM imefanikiwa kuleta mageuzi ya kweli ya kupanua demokrasia nchini, kuendeleza haki za binadamu na haki za msingi za raia wa Tanzania.

Alisema mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi ulipoanza kulikuwa na chama kimoja cha siasa ambacho ni CCM na mwaka 1995 vyama 13 vyenye usajili wa kudumu. 

Idadi hiyo ilibakia hivyo mpaka mwaka 2001 na ilipofika mwaka 2005 kulikuwa na vyama 18 na mwaka huu 2012 vyama hivyo vimefikia 20 vyenye usajili wa kudumu.
Chanzo: Majira