MAISHA YA BINADAMU NA VIUMBE HAI HATARINI RUAHA

Mwandishi wetu JUHUDI za Serikali na wadau wa uhifadhi na mazingira duniani kote za kuuokoa mto Ruaha Mkuu usikauke ni dhahiri sasa zinaan... thumbnail 1 summary
Mwandishi wetu
JUHUDI za Serikali na wadau wa uhifadhi na mazingira duniani kote za kuuokoa mto Ruaha Mkuu usikauke ni dhahiri sasa zinaanza kugonga mwamba baada ya mto huo kuendelea na kasi yake ya kujigeuza kutoka mto wa mwaka mzima kuwa wa msimu.

Kufuatia hali hiyo maisha ya watu na wanyama na viumbe wengine hai katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kwingineko unakopita mto huo yako hatarini ikiwa mto huo utakauka kabisa.

Takribani miaka saba iliyopita mamia ya wafugaji na maelfu ya mifugo iliyokuwa ndani ya eneo oevu la Ihefu waliondolewa na serikali kwa lengo kulinda eneo oevu la Ihefu ambalo ndiyo chanzo kikuu cha mto Ruaha Mkuu lisiharibiwe na wafungaji hao na hivyo kuendelea kupeleka maji katika mto huo.

Ilitarajiwa kwamba baada ya bonde la Ihefu kurejea katika uasili wake,mto Ruaha Mkuu ungetiririsha maji mwaka mzima lakini kuanzia eneo la Lunda,ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha,mto huo umekauka kabisa na hivyo kuzua hofu kubwa.

Mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Ruaha – RUNAPA Stephano Qolli anasema athari za kukauka kwa mto Ruaha Mkuu sasa wameanza kuziona dhahiri na kulaumu kilimo cha umwagiliaji mashamba makubwa upande wa juu wa mto huo maeneo ya wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya.

Mto Ruaha Mkuu unategemewa sana katika uchumi wa Taifa kupitia kilimo, uhifadhi na uzalishaji nishati ya umeme katika bwawa la Mtera na Kitadu na kama isingekuwa juhudi za Wizara ya Nishati na Madini,Taifa hivi sasa lingekuwa katika mgawo mkubwa wa umeme kutokana na hali ya bwawa la Mtera kuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na miaka minne iliyopita.