Mgogoro wa Ziwa Nyasa, Tanzania yapongezwa na Umoja wa Mataifa

Ziwa Nyasa ambalo linawaniwa na Tanzania na Malawi WAKATI Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban K i – m o o n akipongeza msimamo ... thumbnail 1 summary

Ziwa Nyasa ambalo linawaniwa na Tanzania na Malawi
WAKATI Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban K i – m o o n akipongeza msimamo wa Tanzania katika kutafuta majawabu ya amani kuhusu mzozo wa mpaka kati yake na Malawi kwenye Ziwa Nyasa, Rais Joyce Banda wa nchi hiyo ametangaza kwenda mahakamani.
Katika pongezi zake kwa Tanzania juzi, Ban alisema uamuzi wa Tanzania ndiyo njia sahihi na inayokubaliwa kimataifa kutafuta na kupata suluhisho la migogoro ya namna hiyo.
Lakini kwa upande wake, Rais Banda alilitangazia Taifa lake kuwa analipeleka suala hilo katika Mahakama ya Kimataifa (ICJ) ili haki iweze kutendeka, akiilaumu Tanzania kwa alichodai ni kuchora ramani mpya ya Tanzania ikiwa na sehemu ya Ziwa hilo.
Ban alitoa pongezi hizo kwa Tanzania juzi alipokutana kwa mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko hapa, kwa ziara ya siku mbili.
“Juzi nilikutana na Rais Banda wa Malawi na akanielezea mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa na mazungumzo ambayo nchi zenu mbili zinafanya ili kupata ufumbuzi wa amani.
Hii ndiyo njia sahihi na UN inaunga mkono njia hiyo,” Ban alimweleza Rais Kikwete. Rais Kikwete naye alimwambia Katibu Mkuu kuwa Tanzania bado inaamini kwamba njia sahihi ni kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo wa mpaka kwa njia ya mazungumzo.
Alisema: “Wazo la awali la kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili la miaka mingi sana lilitokana na Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika ambaye ni marehemu, ambaye aliniandikia barua ya kutaka nchi zetu zianze mazungumzo kuhusu mzozo huo.Nasi tulikubali.
Hivyo, ndivyo tulivyoanza kuzungumza.” Rais Kikwete alisema Tanzania inaongozwa na msingi mkuu wa mipaka inayopita kwenye maeneo ya maji ambako inakuwa katikati.
“Mpaka kati ya Malawi na Msumbiji kwenye Ziwa hilo hilo, Nyasa, uko katikati ya Ziwa tangu mwaka 1954 wakati nchi hizo zilipokubaliana kusahihisha makosa ya kuweka mpaka huo nje ya Ziwa.
Mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye mto mkubwa zaidi unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa uko katikati ya mto wenyewe,” alisema Rais Kikwete na kuongeza: “Kila mahali ambako nchi zinatengenishwa na maji, mpaka unakuwa katikati ya nchi. Sisi tunadhani hata kwenye mpaka wetu wa Malawi kwenye Ziwa Nyasa ni lazima uwe katikati ya Ziwa.”
Alisema: “Katika hali ya sasa wananchi wetu wanapokunywa maji ya Ziwa Nyasa wanakunywa maji ya Malawi, kila watu wetu wanaposafiri ndani ya Ziwa kufanya shughuli zao wanasafiri kwenye maji ya Malawi.Hili ni jambo linalohitaji majadiliano ya kuliweka vizuri.”
Kauli ya Banda
Banda aliwaambia waandishi wa habari juzi jijini Lilongwe, kwamba suala hili limefika mbali na Malawi sasa itatafuta msaada wa kimataifa kuhakikisha kwamba haki inatendeka, akisema Wamalawi hawawezi kuvumilia usumbufu kila wanapotaka kuvua ndani ya Ziwa hilo.
“Suala hili la Ziwa limefikia hatua nyingine. Nimeamua kulifikisha katika Mahakama ya Kimataifa ili kuamua na kutatua mzozo huu,” Rais Banda alisema.
Banda alifafanua kuwa serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, iliiandikia barua Serikali ya Tanzania juu ya suala la kutoa ramani mpya ambayo inahusisha sehemu ya Ziwa Nyasa.
Alisema mkutano mwingine ambao awali ulikubalika ufanyike Tanzania, ulifutwa baada ya kubaini kwamba Tanzania imetoa ramani mpya, akisema kama itajibu barua hiyo Malawi itaamua ama kuendelea na mkutano huo au la.
“Tuliamua kufuta mkutano huo baada ya kubaini kwamba Tanzania imetoa ramani mpya ikiwa na sehemu ya Ziwa letu. Kama hawatajibu barua yetu tutatafuta njia nyingine,” alisema Rais huyo aliyeingia madarakani mapema mwaka huu baada ya kifo cha Rais Mutharika.
Ban asifu mchakato wa Katiba
Katika hatua nyingine, Ban alisifu na kupongeza uamuzi wa Rais Kikwete wa kuandikwa upya kwa Katiba ya nchi. Aidha, Ban alipongeza hatua ya amani na utulivu uliofikiwa Zanzibar baada ya maridhiano na makubaliano ya kisiasa visiwani humo.
“Rais nakupongeza sana kwa uamuzi wako sahihi na wa busara wa kisiasa wa kuangalia upya Katiba ya sasa ya nchi yako kwa nia ya kutungwa Katiba mpya, kwa sababu hatua hiyo dhahiri itaendeleza utulivu ambao umedumu Tanzania kwa miongo mingi,” Ban alisema.
Ban alimwambia Rais Kikwete kuwa sasa Tanzania na eneo lote la Afrika Mashariki linanufaika na uamuzi mwingine wa busara wa kisiasa wa kutafuta na kupata maridhiano Zanzibar.
Alisifu jitihada zinazofanywa na viongozi wa nchi wa eneo la Maziwa Makuu katika kuleta amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Niliitisha mkutano wa viongozi wa eneo hilo Septemba 27, walihudhuria viongozi wengi akiwamo Rais Joseph Kabila wa DRC na Rais Paul Kagame wa Rwanda, na kuwaeleza kuwa UN inafuatilia kwa makini matukio ya eneo hilo na kuwajulisha kuwa kama wanahitaji msaada wowote wa UN basi sisi tuko tayari,” alisema Ban.
Katibu Mkuu pia alimwomba Rais Kikwete kusaidia maendeleo ya kisiasa Zimbabwe baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chombo Maalumu cha Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu Siasa, Ulinzi na Usalama.
“Kwa nafasi yako ya Mwenyekiti wa Chombo Maalumu cha SADC ni dhahiri kuwa unaweza kuchangia sana naendeleo ya kisiasa ya Zimbabwe,” alimwambia Rais Kikwete ambaye alikubaliana na kauli ya Ban.
Rais alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa uamuzi wa kuandika Katiba mpya unalenga kuwa na Katiba ambayo itaiongoza Tanzania kwa miaka 50 ijayo.
“Baada ya kutumia Katiba yetu nzuri kwa miaka 50 iliyopita, tukaamua kuwa pengine ni vema kuunda Katiba ambayo itatupeleka kwa miaka mingine 50 ijayo. Naamini hili litatusaidia,” alisema Rais Kikwete.