Na Eliya Mbonea, Arusha.
RAIS Jakaya Kikwete, kesho atazindua hadhi ya Jiji la Arusha, baada ya
kukabidhiwa hati rasmi ya kutambulika kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Hati hiyo ilitolewa Agosti 15, 2012, ambapo uzinduzi rasmi sasa unatarajiwa kufanywa katika Mnara wa Mwenge jijini hapa.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo.
Alisema mbali na kuzindua Jiji la Arusha, Rais Jakaya Kikwete, atakuwa na ziara ya kikazi ya siku tatu.
“Rais atazindua Hospitali ya Oltrumet kule Arumeru Magharibi, ataweka jiwe la msingi ujenzi wa Barabara ya Arusha–Minjingu.
“Shughuli
nyingine atakayoifanya akiwa mkoani kwetu, ni kuzungumza na wananchi
katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid hiyo Novemba Mosi,” alisema Mulongo.
Alisema
Novemba 2, 2012, Rais Kikwete atazindua Chuo Kikuu cha Mandela cha
Sayansi na Teknolojia na kisha kutembelea kiwanda cha A to Z.
Alisema
ziara hiyo itakwenda hadi Novemba 3, mwaka huu ambapo atakwenda
kuzindua Shule ya Msingi ya Sokoine, iliyojengwa katika eneo la JWTZ
Monduli.
“Baada ya shughuli hiyo, atakwenda kuweka jiwe la msingi
katika eneo la Nanja Barabara ya Arusha hadi Minjingu,” alisema
Mulongo.
Kwa upande wake, Meya wa Arusha, Gaudence Lyimo, alisema
kupatikana kwa cheti hicho, kunaipa mamlaka iliyokuwa Halmashauri ya
Manispaa ya Arusha kutumia rasmi hadhi ya jiji.
“Hii inatufanya kubadilisha kuanzia nyaraka zote za vitendea kazi, pamoja na Nembo ya Manispaa ambapo sasa tutatumia nembo mpya.
Alisema
Halmashauri hiyo ilianza tangu mwaka 1948, ikiwa ni Halmashauri ya Mji
baada ya kukua kwa mji, ambapo ilipandishwa hadhi na kuwa manispaa mwaka
1980.
Kutokana na kupanuka kwa shughuli katika eneo la kilomita
za mraba 93, Serikali iliamua kupandisha hadhi ya eneo hilo hadi kufikia
kilomita za mraba 2,008.
“Hii ni kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba 341 la Oktoba 14, mwaka 2011,” alisema Meya Lyimo.
Chanzo: Mtanzania