na Joseph Malembeka, Morogoro
KUNDI kubwa la tembo limeibuka katika vijiji vya Kata ya
Bwakila Chini, wilayani Morogoro na kuua watu wawili na kujeruhi watatu
wakiwamo wawili waliojeruhiwa vibaya na kulazwa katika kituo cha afya
Duthumi.
Diwani wa kata hiyo, Pesa Pesa, aliwataja waliouawa kuwa ni mwalimu mstaafu, Thobias Alfani (74) na Milembe Pawa (38).
Alisema waliojeruhiwa ambao sasa wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa
Morogoro ni Dogomisi Makinga (18) na Holo sagala (3) na wengine
walitibiwa na kuruhusiwa.
Alisema kundi hilo la tembo liliibuka alfajiri ya kuamkia juzi
kijijini hapo na kuanza vurumai hiyo kabla hawajadhibitiwa na askari wa
wanyama pori kutoka Hifadhi ya Selous.
Alisema Alfani alikutwa na zahama hiyo akiwa porini kutafuta kuni
ambazo hufanya biashara kijijini hapo huku Pawa alikutwa na zahama hiyo
akiwa njiani na mwanae.
Aliongeza kuwa baada ya watu kupata taarifa ya tukio hilo waliingia mitaani kuwasaka tembo hao.
Akizungumzia hali za majeruhi, Daktari wa Kituo cha Afya Dhutumi,
Japhet Gande, mbali na kukiri kupokea majeruhi hao, alisema
wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi
Chanzo: Tanzania Daima