UNAYAFAHAMU MADHARA YA MABADILIKO YA TABIANCHI?

Kuna madhara mengi yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo jambo la kwanza ni ongezeko la joto duniani, hii ni kuongezeka kwa jot... thumbnail 1 summary


Kuna madhara mengi yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo jambo la kwanza ni ongezeko la joto duniani, hii ni kuongezeka kwa joto katika uso wa dunia.
Mabadiliko ya tabianchi yameongeza sana mioto ya porini, joto kali, ukame wa kutisha na hata kupoteza maisha ya binadamu na viumbe hai.
Madhara mengine ni kuongezeka kwa kina cha bahari mfano mzuri ni katika kijiji cha Gezaulole katika Manispaa ya Temeke ambapo maji yamechukua sehemu kubwa ya kijiji hicho, pia kuna mifano mingi sana kama huu katika fukwe mbalimbali za bahari hapa nchini.
Madhara mengine ni kubadilika kwa misimu ambapo sasa imekuwa ni kitu cha kawaida kuona mvua kubwa ikinyesha wakati wa kiangazi na wakati wa masika kukosa mvua jambo ambalo husababisha mafuriko na ukame mkubwa unaoathiri mfumo wa kilimo nchini.
Kuonea kwa jangwa pia ni moja ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi mfano mzuri ni mikoa ya Dodoma, Singida na Shinyanga iko katika hatari ya kugeuka jangwa kutokana na kuwepo kwa ukame mkubwa sambamba na uharibifu wa mazingira unafanywa na wakazi wa maeneo hayo.
Madhara mengine ni kuongezeka kwa magonjwa hasa kwa Tanzania ni ugonjwa hatari wa malaria ambapo katika mikoa kama Kilimajaro na Iringa ambazo zilitajwa kuwa na kiwango kidogo cha wagonjwa wa malaria katika miaka ya nyuma lakini sasa kutokana na kuongezeka kwa joto duniani watu wanaougua malaria wameongezeka.
Pia mabadiliko ya tabia nchi yamepunguza pato la taifa hasa kutokana na kuathiri sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia pato la taifa na kukuza maendeleo kwa ujumla.
Hata hivyo hatujachelewa katika katika kuinusuru Tanzania yetu na dunia kwa ujumla kwani kuna kitu tunaweza kufanya, soma makala ijayo itaeleza njia za kupambana ama kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambazo kila mmoja wetu kwa nafasi yake anaweza kuzichukua kunusuru maisha ya kizazi cha sasa na cha baadae.