Kikwete aagiza Moshi iwe Jiji ifikapo 2015

Moshi RAIS Jakaya Kikwete ameagiza uongozi wa Manispaa ya Moshi na ule wa Halmashauri ya Moshi Vijijini kukaa meza moja kuzungungumza na ... thumbnail 1 summary
Moshi
RAIS Jakaya Kikwete ameagiza uongozi wa Manispaa ya Moshi na ule wa Halmashauri ya Moshi Vijijini kukaa meza moja kuzungungumza na kukubaliana ili mji wa Moshi uwe Jiji ifikapo 2015.
Agizo hilo la Rais Kikwete linatokana na uongozi wa Manispaa ya Moshi (MMC) kuwashtaki wenzao wa Moshi Vijijini (MDC) kwa Rais kuwa, ndiyo kikwazo cha kupanuka kwa mji huo na kuwa Jiji.
Mkurugenzi wa MMC, Bernadette Kinabo alimweleza Rais Kikwete juzi kuwa, Mji wa Moshi umeshindwa kuwa Jiji kutokana na MDC kukataa maombi yao ya kutaka mji upanukie Moshi Vijijini.
“Tunashindwa kuwa Jiji kwa sababu kwa visheni ya manispaa mwaka huu tulipaswa kuwa jiji, tulitaka kupanuka kutoka eneo la kilomita 58 za mraba za sasa hadi kilomita 142,” alisema.
Hata hivyo, Kinabo alisema kutokana na utamaduni wa kumiliki mashamba madogomadogo maarufu kama Vihamba, MDC wamekataa maombi ya MMC ya kupanukia eneo la halmashauri hiyo.
“Halmashauri ya Moshi (MDC) wamekataa kufikiria maombi yetu ambayo kila mara tumekuwa tukiyapeleka, tutaendelea kuyapeleka hadi hapo tutakapopata eneo la kupanukia,” alisema Kinabo.
Ingawa Kinabo hakutaja vijiji vya Moshi Vijijini vinavyopaswa kuingia katika Manispaa ya Moshi, lakini chini ya mpango wa Moshi kuwa jiji, vijiji vinane vinapaswa kuingia mjini.
Vijiji hivyo ni Rau River, Chekereni, Mabogini, Mvuleni, Mtakuja, Kindi Msasani, Chekereni na Mandaka Mnono vilivyopo Kata za Kahe, Mabogini, Kindi na Old Moshi Magharibi.
Kinabo alitoa kilio hicho alipotoa taarifa yake wakati wa sherehe za uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa Moshi.
Alisema Mji wa Moshi unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kufungwa kwa viwanda 15, ujenzi holela pembezoni mwa mji na mabadiliko ya tabianchi.
Akijibu taarifa hiyo, Rais Kikwete alizitaka halmashauri hizo mbili kuendelea na mazungumza na yalenge kuhakikisha Mji wa Moshi unakuwa jiji ifikapo mwaka 2015.
Chanzo: Mwananchi