Mtazamo wangu: Jamii ipewe elimu ya utunzaji mazingira

Lucy Valentine. WIKI iliyopita kulikuwa na maadhimisho ya miaka 67 ya mazingira yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN), ambapo kwa hapa ... thumbnail 1 summary
Lucy Valentine.
WIKI iliyopita kulikuwa na maadhimisho ya miaka 67 ya mazingira yaliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN), ambapo kwa hapa nchini yalifanyika jijini Dar es Salaam.
Katika maadhimisho hayo kulizungumzwa mambo mengi likiwamo suala la uchafuzi wa mazingira, ambalo kwa sasa ni kubwa na linapaswa kupewa kipaumbele zaidi.
Kama tujuavyo, katika mazingira tunayoishi tumezungukwa na vitu mbalimbali ikiwamo mito, miti, maziwa, bahari na vinginevyo; hivyo tunapaswa kuyatunza kwa faida yetu.
Kwa mtazamo wangu, jamii inayopenda mazingira huyatunza kwa kuyaweka safi, lakini kwa hapa nchini hususani katika Jiji la Dar es Salaam, watu wamekuwa wakiyatumia vibaya kwa kutupa takataka ovyo.
Hapo awali mazingira yalikuwa yanaridhisha kidogo, lakini kwa sasa yamekuwa machafu zaidi.
Mazingira yamekuwa machafu kutokana na ongezeko la watu, hasa katika maeneo ya mijini ambako huchafuliwa kutokana na umwagaji wa maji machafu kutoka viwandani kwenda katika makazi ya watu, moshi wa viwanda na ukataji wa miti pasipo mpangilio.
Kiuhalisia, ukataji hovyo wa miti una madhara mbalimbali, ikiwamo kusababisha mmomonyoko wa udongo ambao husababisha jangwa na mvua kutokunyesha kwa wakati.
Katika baadhi ya sehemu, hali ya mmomonyoko wa udongo na kutokuwepo kwa mvua vimeanza kujitokeza, sababu kubwa ikiwa ni kutokutunza mazingira yetu.
Kwa mtazamo wangu, uchafuzi wa hali ya hewa kutokana na viwanda, kunasababisha mazingira kuwa na muonekano mbaya ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa hewa, hali inayoweza kusababisha watu kuugua maradhi kama kifua kikuu (TB), kikohozi na hata kusababisha vifo.
Inasikitisha katika Jiji la Dar es Salaam kuona watu na heshima zao wakifungulia vyoo wakati wa mvua ili maji machafu yachanganyike na maji ya mvua, hali inayosababisha magonjwa ya kichocho, kipindupindu na kuhara.
Kwa mtazamo wangu, ufunguliaji huo wa vyoo unatokana na ukosefu wa elimu katika jamii, hivyo ni vema viongozi wakiwamo wa serikali za mitaa kutoa somo kuhusu suala hilo.
Pamoja na mazingira kuwa machafu, inabidi wananchi wabadilike na wajue kwamba jukumu lao ni kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Kwa watu wanaojali afya zao na za wengine, huhamasisha watu kuyaweka mazingira katika hali ya usafi, lakini pia hutoa elimu juu ya madhara yanayoweza kupatikana kutokana na uchafuzi wa mazingira.
Hata hivyo, jamii inatakiwa kutumia mapipa yanayowekwa barabarani kwa ajili ya kuhifadhia taka na wazoa taka nao wanapaswa kuwa makini katika kuangalia vyombo hivyo kama vimejaa na kuviondoa ili kuepuka taka kuzagaa zitakazotupwa kutokana na kujaa kwa vifaa vya kuzihifadhia.
Pamoja na hayo, katika utunzaji wa mazingira kuna vitu ambavyo mtu anapaswa kuzingatia kujiepusha navyo kama ukataji miti, kutupa taka ovyo na kila mmoja ajijengee tabia ya kupanda miti.
Pia viwanda vitengewe sehemu maalumu mbali na makazi ya watu, kwa ajili ya kudhibiti harufu mbaya na uchafuzi wa hewa katika makazi ya watu.
Elimu ya utunzaji wa mazingira nayo inatakiwa kufundishwa shuleni ili jamii kwa ujumla inufaike kutokana na mazingira hayo kwa kizazi cha sasa na baadaye.
Aidha, serikali inatakiwa idhibiti utengenezaji wa mifuko ya plastiki, ambayo awali waliikataza, lakini sasa inaonekana kuzagaa tena mitaani.
Kutokana na elimu itakayotolewa, wananchi wanapswa kuifuata na kutekelezwa ili kuepuka kusukumwa na sheria itakayowekwa kwa faida yao wenyewe.
Kwa mtazamo wangu, ile kasumba ya kwamba serikali ndiyo inapaswa kutunza mazingira tuiondoe, kwani kila mtu anapaswa kusimamia jukumu hili.
Wananchi tuungane na tujitume katika kutekeleza wajibu wetu kwani suala la mazingira ni letu sote.
0769 679695  
Chanzo: Tanzania Daima