Zijue hifadhi za taifa na wakati wa kutembelea

Gordon Kalulunga. WATANZANIA wengi kutokana na mazoea, hudhani wanaotakiwa kutembelea hifadhi za taifa ni watalii wa nje ya nchi. Waz... thumbnail 1 summary
Gordon Kalulunga.
WATANZANIA wengi kutokana na mazoea, hudhani wanaotakiwa kutembelea hifadhi za taifa ni watalii wa nje ya nchi.
Wazawa wengi wameshindwa kujitokeza kwa wingi kutembelea hifadhi hizo kutokana na sababu mbalimbali.
Moja ya sababu hizo ni pamoja na hofu ya viingilio wakifika katika hifadhi hizo jambo ninaloamini kuwa baada ya kusoma makala hii, wengi wetu tutabadili fikra na kujitokeza katika vivutio vya utalii vilivyopo kila pembe ya nchi yetu.
Willy Cosmas mkazi wa Arusha, jiji lenye vivutio vya utalii, anasema licha ya kuishi jijini hapo kwa muda wa miaka saba, hajaweza kutembelea vivutio vilivyopo ingawa huwa anaona watalii wakiwa kwenye magari wakipelekwa katika mbuga na vivutio vingine.
John Tarimo, mkazi wa Usa River mkoani Kilimanjaro anasema licha ya kutoweza kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo nchini, ana uwezo wa kumwelezea mtu/mgeni baadhi ya vivutio na hata mahala vinakopatikana.
Baadhi ya vivutio vinavyosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa la Tanzania (TANAPA) ni Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Gombe, Katavi, Mlima Kilimanjaro, Mahale, Mikumi, Manyara, Ruaha, Rubondo, Serengeti, Saadan, Tarangire, Udzungwa, Kitulo, Mkomazi na Saanane.
Katika hifadhi hizo, unapotembelea kuna tozo zake za kuingilia hifadhini ambapo mtu mzima analipa sh 1,500 na sh 500 kwa mtoto chini ya miaka 16.
Arusha
Kaimu Mkurugenzi wa TANAPA, Ahmed Mbugi, anasema Hifadhi ya Taifa ya Arusha ina ukubwa wa kilomita za mraba 328.4 na iko umbali wa kilomita 62 (kiasi cha mwendo wa saa moja kwa gari) kutoka mji wa kitalii wa Arusha.
“Hifadhi hii ina maeneo matatu muhimu ambayo ni Bonde la Ngurdoto (Ngurdoto Crater), maziwa ya Momella ambayo kila moja hutoa mandhari tofauti pamoja na Mlima Meru wenye urefu wa mita 4,566 hali inayoifanya hifadhi kuwa na mazingira ya baridi,’’ anasema Mbugi.
Ikumbukwe kuwa hifadhi hii ni maarufu kwa wanyama jamii ya tumbili wajulikanao kama mbega weusi na weupe.
Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni twiga, pundamilia, nyati na digidigi.
Unaweza kuwaona chui wakibarizi katika vivuli vya matawi ya miti inayokingwa na maanguko ya maji, huku makundi kadhaa ya batamaji yakitafuta wadudu katika maziwa ya Momella.
Zaidi ya aina 400 za ndege wamethibitika kupatikana ndani ya hifadhi hii.
Safari za miguu na kupanda Mlima Meru ni moja ya burudani muhimu katika hifadhi ambapo mpandaji anahitaji kati ya siku tatu hadi nne za kupanda mlima.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kati ya Juni na Februari.
Gombe
Hii ni hifadhi ndogo kuliko zote nchini ikiwa na jumla ya kilometa za mraba 52, lakini ina umaarufu mkubwa unaotokana na kuwa na wanyama aina ya sokwe.
Gombe ni moja ya makazi machache yaliyosalia ya sokwe duniani. Ipo kilomita 16 kaskazini mwa mji wa Kigoma. Hifadhi hii ni ukanda mwembamba wa msitu wa mlima unaokatizwa na miteremko mikali inayoingia katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni kima wenye mikia myekundu na wa rangi ya bluu.
Unaweza kwenda kutembelea hifadhi hii kwa ndege za abiria au za kukodi kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma mjini na baadaye kwa boti hadi Makao Makuu ya Hifadhi.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni Julai hadi Oktoba, kipindi cha kiangazi kwani sokwe hawapendi kutembea nyakati za mvua.
Katavi
Hifadhi ya Taifa ya Katavi ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 4,471, iko juu ya uwanda mpana wa mafuriko kusini magharibi mwa Tanzania katika Mkoa wa Katavi - zamani Rukwa.
Mandhari kuu katika hifadhi hii ni maeneo yenye majimaji, majani, mimea mithili ya mitende pamoja na Mto Katuma.
Inasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya mamba na viboko na ni kawaida kuyaona makundi makubwa ya tembo wakila majani katika mabwawa huku miili yao ikiwa imefunikwa na maji na magugu.
Mahale
Hifadhi hii inaundwa na vilima vilivyojipanga na kufunikwa na misitu minene, ina kilomita za mraba 1,613.
Kama ilivyo hifadhi ya jirani ya kaskazini ya Gombe, hifadhi ya milima ya Mahale ni makazi ya jamii adimu zilizobakia za sokwe barani Afrika.
Mabaki ya matunda yaliyoliwa na kinyesi kibichi ni miongoni mwa alama zitakazokuongoza mgeni hadi kuwafikia viumbe hawa katika misitu iliyopo katika mlima huo na hifadhi hii ipo magharibi mwa Tanzania ikiwa inapakana na Ziwa Tanganyika.
Ukifika hapo utaona sehemu ya asili ya watu wa kabila la Watongwe walipokuwa wakiabudia mizimu yao milimani, kisha kurudi ziwani na kujitumbukiza kwenye maji baridi na maangavu.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ni kipindi cha kiangazi cha Mei na Oktoba.
Ziwa Manyara
Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ni maarufu kwa simba wanaopanda miti. Ziwa lipo ndani ya hifadhi ambayo ina ndege zaidi ya aina 400 wanaovutia, wakiwemo aina ya korongo ambao huonekana kama pazia kubwa jeupe.
Idadi kubwa ya wanafunzi hapa nchini wanatembelea hifadhi hii na kujionea maajabu yaliyopo ambapo ni pamoja na wanyama kama simba, nyati, tembo, nyani, chui, pundamilia na wengine wanaokula majani.
Pia kuna chemchem za maji moto yanayobubujika kutoka ardhini bila kukauka kwa mamilioni ya miaka.
Hifadhi hii ipo umbali wa kilomita 126 kutoka Arusha mjini na wakati mzuri wa kutembelea ni kuanzia Juni hadi Desemba.
Ruaha
Hifadhi ya Ruaha ndiyo kubwa kuliko zote Tanzania; ina ukubwa wa kilomita za mraba 20,226 na ni ya pili kwa ukubwa katika Bara la Afrika baada ya hifadhi ya Kafue iliyopo nchini Zambia.
Ni maarufu kwa kuwa na wanyama aina ya kudu wakubwa na wadogo ambao hupatikana kwa wingi.
Hustawi wa hifadhi hii unategemea Mto Ruaha wenye aina mbalimbali za samaki, mamba na viboko.
Wanyama kama pofu na swala hunywa maji katika mto huu, pia kuna mawindo makubwa ya wanyama wakali wakiwemo simba, chui, mbweha, fisi na mbwa mwitu.
Pia eneo hili tembo hukusanyika kwa wingi kuliko eneo lolote la hifadhi zilizopo katika nchi za Afrika Mashariki.
Katika hifadhi hii kuna magofu yanayosadikiwa kuwa yalikuwa makazi ya watu wa kale katika Kijiji cha Isimila, umbali wa kilomita 120 kutoka Iringa. Magofu haya ni miongoni mwa historia ya kale barani Afrika.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ili kuangalia wanyama wakubwa ni wakati wa kiangazi kuanzia Mei hadi Desemba, lakini kuangalia ndege na maua wakati wa masika ni Januari hadi Aprili.
Rubondo
Hifadhi hii ni kisiwa ambacho kipo pembezoni mwa Ziwa Victoria, ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani likiwa linazungukwa na nchi za Tanzania, Uganda na Kenya.
Kisiwa hiki kinachoundwa na visiwa tisa vidogo vidogo ni makazi na mazingira ya kuzaliana samaki wakiwemo sato na sangara wenye uzito wa kilo hadi 100.
Wanyama wanaopatikana katika hifadhi hii ni viboko, pongo, nzohe, fisimaji, mamba na pimbi ambao huwa wanabadilishana makazi na wanyama wengine waliohamishiwa katika hifadhi hii kama sokwe, tembo, mbega na twiga.
Wakati mzuri wa kutembelea ni wa kiangazi kuanzia Juni hadi Agosti.
Saadan
Hifadhi hii ipo ufukweni mwa Bahari ya Hindi na ni pekee Afrika Mashariki inayoungana na bahari. Ipo umbali wa kilomita 100 kaskazini magharibi mwa Dar es Salaam na umbali kama huo kusini magharibi mwa bandari ya Tanga.
Ilianzishwa kama pori la akiba mwaka 1960 na ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya taifa mwaka 2005.
Katika hifadhi hii kuna simba, chui, fisi, tumbili, swala na ngedele.
Mbali na kuona wanyama katika hifadhii, pia mtalii hupata nafasi ya kuogelea.
Kipindi cha kutembelea hifadhi hii ni wakati wote wa mwaka ingawa wakati wa masika barabara zinaweza kutopitika kirahisi.
Udzungwa
Hifadhi hii ya Milima ya Udzungwa ina hazina nyingi za mimea, ndege na wanyama ambazo hazipatikani sehemu nyingine duniani.
Kati ya aina sita za jamii ya nyani wanaopatikana katika hifadhi hii, mbili hupatikana katika hifadhi hii pekee. Pia kuna mbega mwekundu wa Iringa, ambaye alikuwa hajulikani hadi mwaka 1979.Kivutio kikubwa zaidi ni Mto Sanje unaotoa maporomoko ya maji yenye urefu wa mita zipatazo 170 yakianguka kupitia msituni na kutua mithili ya ukungu bondeni.
Kitulo
Awali hifadhi hii ilijulikana kwa jina la Elton Plateau baada ya mvumbuzi Fredrick Elton kupita eneo hili mwaka 1870; mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) lilichukua eneo hili kwa ajili ya kilimo cha ngano na ufugaji wa kondoo.
Baadaye likageuzwa kuwa shamba la ng’ombe ambalo lipo hadi leo.
Mwaka 2005 Kitulo ikatangazwa kuwa hifadhi ya taifa yenye maua aina mbalimbali na zaidi ya aina 30 hupatikana hapo pekee.
Kupitia makala hii ni muhimu kupata mwamko wa kutembelea hifadhi zetu kwa ajili ya kujifunza historia na kujua mambo mbalimbali yanayopatikana nchini.
0754 440749 kalulunga2006@yahoo.com www.kalulunga.blogspot.com 
Chanzo: Tanzania Daima