Habari kwa kina: Ndege za abiria zagongana Z’bar

Ndege mbili za abiria ziligongana juzi jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wakati moja ikielekea kupaa na nyin... thumbnail 1 summary
Ndege mbili za abiria ziligongana juzi jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wakati moja ikielekea kupaa na nyingine ikiwa imeegeshwa.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, ndege ya Shirika la Ndege la Oman iliyokuwa ikijiandaa kupaa iliigonga ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia iliyokuwa imeegeshwa.
Katika ajali hiyo iliyotokea saa 10 jioni, ndege ya Oman iligonga sehemu ya bawa la ndege ya Ethiopia.
Ajali hiyo ilisababisha taharuki kwa abiria waliokuwamo kwenye ndege hizo.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Rashid Seif Suleiman alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa tayari uchunguzi umeanza ili kufahamu chanzo chake.
“Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Zanzibar wameanza kufanya uchunguzi kujua chanzo cha ajali hiyo,” alisema Waziri Seif.
Alisema ndege ya Oman ilikuwa imebeba abiria 150 tayari kwa safari ya kuelekea Dar es Salaam.
Baada ya ajali hiyo, mafundi waliikagua ndege ya Oman na kubaini kuwa haikuwa imeathirika na kuruhusiwa kuendelea na safari saa tatu usiku, juzi.
Ndege ya Ethiopia iliondoka jana saa tatu asubuhi baada ya kufanyiwa matengenezo kwenye ncha ya bawa.
“Ni mapema kueleza chanzo chake, tuwaachie wataalamu wafanye kazi ya uchunguzi na baadaye tutajua,” alisema Waziri Seif na kuongeza: “Siwezi kusema uchunguzi utachukua muda gani lakini ni jambo linalohitaji kufanyika haraka na wataalamu wetu wapo kazini.”
Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko ya siku nyingi kwamba uwanja huo unakabiliwa na tatizo la ukosefu wa michoro ya kuongoza ndege zinapoingia na kutoka.
Chanzo: Mwananchi