Majiko bunifu yapunguza uharibu mazingira

WANANCHI wanaoishi maeneo ya milimani mkoani Morogoro wamesema mpango wa matumizi ya majiko bunifu yamewasaidia kukabiliana na vitendo vy... thumbnail 1 summary
WANANCHI wanaoishi maeneo ya milimani mkoani Morogoro wamesema mpango wa matumizi ya majiko bunifu yamewasaidia kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira vilivyokuwa vikiendelea katika milima ya Uluguru.
Wananchi hao  walitoa kauli hiyo walipozungumza na Balozi mdogo wa Norway nchini Tanzania, Berit Kristin Tvete Exper, aliyetembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali ya Norway kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Milima ya Tao la Mashariki (Eastern Arc).
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, Estere Anaclet na Victoria Aloyce, walisema utaalamu huo unaotumika ni muhimu kwani umesaidia kutunza na kuhifadhi mazingira.
Akiwa katika ziara ya siku mbili balozi huyo alitumia fursa hiyo kujionea namna majiko hayo yaliyotengenezwa kwa utaalam wa  kikundi cha kuhifadhi mazingira cha Meca, kwa ufadhili wa Eastern Arc, yanavyofanya  kazi, kujionea vitalu vya miti, na kupanda miti kwenye milima ya Uluguru.
Balozi Tvete pia alitembelea wilaya ya Mvomero katika msitu wa hifadhi ya mazingira asilia  wa Vikingu, ulioko kwenye safu za milima ya Nguru na kuona jinsi msitu huo ulivyohifadhiwa kwa kushirikiana na wananchi.
Katika wilaya ya Kilombero, balozi huyo alitembelea hifadhi ya taifa ya milima ya Udzungwa na kujionea vivutio mbalimbali.
Mkurugenzi mtendaji wa mfuko huo, Francis Sabuni, alisema kupitia wahisani mbalimbali ikiwemo serikali ya Norway, wamekuwa wakifadhili miradi ya uhifadhi kwenye hifadhi za taifa na maeneo mengine kuanzia ukanda wa kusini hadi kaskazini ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.

Chanzo: Tanzania Daima