Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro: Mbunge Msigwa amtuhumu Balozi Kagasheki kwa ufisadi

MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), amemlipua Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kwa madai kuwa ... thumbnail 1 summary
MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), amemlipua Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kwa madai kuwa amekuwa akitumia mamlaka yake vibaya na kusababisha ufisadi kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Hatua hiyo ya Mchungaji Msigwa, imekuja baada ya kubainika kuwa Balozi Kagasheki ametoa msamaha kwa kugawiwa vitalu kwa Kampuni za Leopard Tours Ltd, Maasai Sanctuaries na Ndutu Oloololo, ambavyo vilikuwa nje ya mpango wa vitalu vya mamlaka kisheria.

Akizungumza mjini hapa jana, Msigwa, alisema Kagasheki aliiandikia barua Mamlaka iweze kuipa Kampuni ya Leopard hekari tano kwa kiasi cha Dola 30,000 za Marekani badala ya Dola 60,000 za Marekani kwa mujibu wa utaratibu zilizowekwa kisheria.

Pamoja na hatua hiyo, alisema tangu alipoingia katika wizara hiyo, Kagasheki alivunja Bodi ya Mamlaka ya Ngorongoro na kushindwa kuunda bodi nyingine, hali ambayo amezidi kuweka mazingira ya ufisadi na upendeleo.

Katika barua hiyo ambayo MTANZANIA Jumatatu inayo, yenye kumbukumbu namba 315/319/01 B na huku katibu mkuu pamoja na mhifadhi wa Ngorongoro, Kagasheki, ameisaini na kutoa maelezo hayo.

Alisema kutokana na nyaraka walizozinasa, wamebaini kuwa Kagasheki ameshindwa kueleza maslahi binafsi aliyonayo hasa baada ya kuiagiza mamlaka hiyo kuipatia fedha taasisi ya Catherine Foundation kinyume na utaratibu wa utoaji misaada.

“Ni wazi kabisa hatua ya Kagasheki kufanya uamuzi huu bila kuzingatia sheria na kanuni za ugawaji wa vitalu, ameshiriki kwa makusudi kuivunja sheria ikiwamo kushusha viwango vya ulipaji wa vitalu kwa vilivyowekwa kisheria bila kutoa tangazo la serikali.

“Ama kujua au makusudi kwa kutokujua, ameshindwa kujua kwamba ana maslahi binafsi na Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Arusha, Catherine Magige (CCM) ambaye ni mke wake.

“Kwa kupitia taasisi ya Catherine Foundation, alipata msaada wa shilingi milioni kumi kutoka katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hali ya kuwa kisheria alitakiwa kupewa shilingi milioni mbili kwa kuwa hiki ndicho kiwango cha utoaji msaada wa kijamii kwa mamlaka hii.

“Dokezo la maombi ya msaada huo linaonyesha kuwa, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitoa mapendekezo mara mbili, kwanza kwa kupitia Manager of Community Development (MCD),” alisema Msigwa.

Alisema kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii ya Ngorongoro, taasisi hiyo ilitakiwa kufikiriwa upya kulingana na maombi waliyowasilisha kuzidi kiwango cha Sh milioni nane zaidi badala ya Sh milioni mbili.

Alisema Kambi ya Upinzani inataka kujua Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ngorongoro alitumia kigezo gani kuilipa taasisi hiyo ambayo alidai ina uhusiano wa kifamilia na Balozi Kagasheki.

“Kambi rasmi ya upinzani inapinga ukiukwaji huu wa sheria unaofanywa na Kagasheki ambaye amepewa mamlaka ya kusimamia sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa letu na inalaani kwa nguvu zote upendeleo unaotokana na maslahi binafsi kati ya Waziri na Magige,” alisema Msigwa.

Kutokana na tuhuma hizo dhidi yake, gazeti hili lilimpata Kagasheki ambapo alisema Msingwa amezua uongo wenye lengo la kumchafua kwa jamii.

“Ninachotaka kusema ni uongo wa kuzua, ila ikifika wakati nitasema tu na kutoa ufafanuzi wa kina na si kwa Ngorongoro bali hata kwa hifadhi nyingine pia,” alisema Kagasheki.

Katika hatua nyingine, Magige, alizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu na alikanusha madai ya Msigwa na kusema kuwa anamkabidhi Mungu kwa sasa.

“Kaka yangu msaada nilioomba umefuata sheria na si kwenda kama Catherine, ila ninachotaka kusema kuwa Msigwa ana lengo la kumchafua Waziri Kagasheki. Hata nilipoomba msaada huu sikutaka kiasi cha fedha.

“Si hilo tu kama ni siasa za kuchafuana na afanye tu ila yana mwisho na taasisi yangu imekuwa ikipita na kuomba misaada katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi na si kwa kutumia jina la mtu zaidi ya kuisadia jamii hasa walemavu, yatima na wazee,” alisema Magige.


Chanzo: Mtanzania