MAMLAKA YA WANYAMAPORI KUWA SULUHISHO LA WANYAMA WALIOKO HATARINI KUTOWEKA

Serikali imesema kuwa uanzishwaji wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori nchini kutasaidia kuokoa wanyamapori walioko hatarini kutoweka. Hayo... thumbnail 1 summary
Serikali imesema kuwa uanzishwaji wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori nchini kutasaidia kuokoa wanyamapori walioko hatarini kutoweka.

Hayo yalisema na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof Alexander Songolwa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Maimuna Tarishi, alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa taaluma mbalimbali nchini waliokutana leo jijini Dar es Salaam kujadili na kutoa mapendekezo ya kuimarisha utendaji wa mamlaka mpya ya usimamizi wa wanyamapori.

Prof Songolwa alisema sekta ya wanyamapori ina changamoto nyingi zinazoathiri uwezo wa serikali wa uhifadhi wanyamapori na mazingira yake kutokana na mfumo wa usimamizi uliopo sasa kutoiwezesha serikali kukabiliana ipasavyo na changamoto hizo kwa ufanisi.

Alisema ili kukabiriana na changamoto hizo Serikali imeamua kubadiri mfumo wa usimamizi na uendelezaji wa sekta ndogo ya wanyamapori kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi.

Aliongeza kuwa mfumo uliopo hivi sasa, Idara ya Wanyamapori inafanya kazi za urekebu, uratibu na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori hali iliyoifanya serikali kuanza mchakato wa uanzishwaji wa mamlaka mpya ya uhifadhi wa wanyamapori ili kutenganisha majukumu hayo.

Alisema katika utenganisho huo, Idara na Wizara itabaki na majukumu mawili ambayo ni urekebu na uratibu na mamlaka itakuwa na jukumu la usimamizi wa rasilimali za wanyamapori.

Prof Songolwa alisema kutokana na umuhimu wa mamlaka hiyo, wadau wasisite kutoa maoni yatakayosaidia kuundwa kwa mamlaka itakayokidhi haja ya serikali ya uhifadhi wa wanyamapori nchini.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Dkt. Simon Mduma aliwataka wadau kujadili kwa kina rasimu za Sheria na Muundo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori pamoja na marekebisho ya sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ili maamuzi ya kimuundo na kisheria yatakayofanywa yawe shirikishi na kwa manufaa ya uhifadhi nchini.

Mchakato huu wa uundwaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori unatekeleza agizo la Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009, ambayo inaitaka Wizara kuanzisha mamlaka hiyo. Mchakato huo umepangwa kukamilishwa Novemba, 2013 baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sheria husika