RAIA wa China, Chen Weitao, dereva wa
Kampuni ya ujenzi ya Chico inayotengeneza barabara ya Musoma-Mwanza, amekamatwa
na askari wa Kikosi cha Kudhibiti Ujangili akiwa na mfupa uliokauka wa mguu wa
tembo.
Weitao alikamatwa juzi, majira ya saa
sita mchana, eneo la Nyasura katika mji mdogo wa Bunda.
Ofisa mmoja wa kikosi hicho Kanda ya
Serengeti ambaye hakutaka kutajwa jina alisema walipata taarifa kutoka kwa raia
mwema.
Alisema baada ya kupata taarifa hiyo
walikwenda moja kwa moja eneo hilo na kumkuta Weitao akiwa na gari T 340 BBR na
baada ya kulikagua walikuta mfupa huo ukiwa kwenye sehemu ya kutunzia spana.
Alisema walimkamata raia huyo wa
China aliyekuwa na msaidizi wake aitwaye, Michael Renatus, na kuwapeleka kituo
cha polisi ambako waliwaweka chini ya ulinzi na kuwahoji.
Raia huyo wa China alidhaminiwa juzi
baada ya kukabidhi hati yake ya kusafiria katika Kituo cha Polisi Bunda na
kupewa gari lake ingawa ataendelea kuhojiwa na kikosi hicho.
Hii ni mara ya nne sasa kwa Wachina
hao kukamatwa na nyara za serikali tangu waanze kujenga barabara hiyo, ambapo
mwaka jana walikamatwa na vipande vya meno ya tembo katika kambi yao iliyopo
Sabasaba.
Polisi wilayani hapa wamekiri
kukamatwa kwa Mchina huyo na kudai suala hilo linasimamiwa na Kikosi cha Kuzuia
Ujangili Kanda ya Serengeti, ambao kwa hivi sasa wana wanasheria wao ambao
wanaandaa mashitaka na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hao.
Chanzo: Tanzania Daima