Miss Utalii kumtangaza kimataifa nyati wa ajabu hifadhi ya Ngorongoro

MISS Utalii Tanzania 2013, Hadija Mswaga, amesema kupatikana kwa nyati mweupe wa ajabu na pekee duniani katika hifadhi ya Ngorongoro mkoani... thumbnail 1 summary
MISS Utalii Tanzania 2013, Hadija Mswaga, amesema kupatikana kwa nyati mweupe wa ajabu na pekee duniani katika hifadhi ya Ngorongoro mkoani Manyara, ni chachu na kichocheo cha pekee kwake katika mpango mkakati wa kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa.

Mswaga alisema kwa kuanzia ameamua kuanza kampeni hiyo kupitia mashindano ya dunia ‘Miss Tourism World 2013’, yatakayofanyika huko Equatorial Guinea Oktoba 12.

Alisema kupatikana kwa nyati huyo wa ajabu ambaye hapatikani sehemu nyingine yoyote duniani, wakati huu ambao anakwenda katika mashindano hayo ya dunia, imekuwa ni fursa ya pekee kwa Tanzania, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kwake, kuithibitishia dunia kuwa Ngorongoro Crater ni eneo la ajabu la asili la dunia barani Afrika.

Mswaga alisema Ngorongoro Crater na Hifadhi nzima ya Ngorongoro ni tunu ya taifa la Tanzania na hazina ya dunia, ambayo inapaswa kuenziwa na kuitangaza kwa nguvu zote, ili iweze kuchangia zaidi uchumi na pato la taifa.

“Naupongeza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kwa jitihada zake za kukuza utalii na kupambana na majangili; nawaomba kuimarisha na kuongeza mapambano na vita dhidi ya ujangili ili kuhakikisha kuwa hawamdhuru nyati huyo wa ajabu na wanyama wengine katika hifadhi hii,” alisema Mswaga.

Wafanyakazi wa hifadhi hiyo, mwishoni mwa wiki wakiwa katika basi la mamlaka wakienda kazini, walimshuhudia nyati huyo akiwa na kundi la wenzake kandokando ya barabara, jambo ambalo liliwavutia na dereva wa basi hilo kulazimika kusimamisha kutoa fursa kumshuhudia na baadhi yao kupiga picha kwa simu zao na kamera walizokuwa nazo.


Mswaga ameushukuru uongozi wa Ngorongoro, kwa kumpa DVD zaidi ya 100 za hifadhi hiyo, ambazo atakwenda kuzigawa kwa washiriki wote 126 na vituo vya televisheni vya nchi zao katika mashindano hayo ya dunia. 

Aliongeza kuwa baada ya kurejea atazunguka nchi nzima na nyingine duniani kuitangaza Ngorongoro kwa kushirikiana na uongozi wa Miss Tourism Tanzania Organisation na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.